Yanga yarejea kileleni, Aziz KI atupia

Muktasari:
- Yanga ambayo mastaa wake kadhaa walikosekana kwenye mchezo huu kutokana na sababu mbalimbali, imefikisha pointi 46 zikiwa ni mbili mbele ya Azam ambayo ina pointi 44, lakini ikiwa nyuma kwa michezo mitatu.
Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kishindo baada ya jana kuichapa Namungo FC mabao 3-1, katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi.
Yanga ambayo mastaa wake kadhaa walikosekana kwenye mchezo huu kutokana na sababu mbalimbali, imefikisha pointi 46 zikiwa ni mbili mbele ya Azam ambayo ina pointi 44, lakini ikiwa nyuma kwa michezo mitatu.
Mwanzoni haikuonekana kama ingekuwa ni mechi yenye idadi kubwa ya mabao lakini dakika tisa tu za kipindi cha pili zilitosha kubadilisha kila kitu ambazo zilitumiwa na Yanga kupata mabao yake matatu kupitia kwa Mudathir Yahya, Clement Mzize na Stephane Aziz Ki.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko kila moja ikiwa haijaona lango la mwenzake, ubao wa matokeo ulianza kubadilika katika dakika ya 53 baada ya Mudathir ambaye amekuwa kwenye kiwango cha juu msimu huu kuipatia timu yake bao la kuongoza akimalizia vyema kwa shuti la mguu wa kulia la Aziz Ki.
Bao hilo ni kama liliipa Yanga shauku ya kusaka mabao zaidi na juhudi zao zililipa katika dakika ya 57, ilipopata la pili kupitia kwa Clement Mzize.
Mzize alifunga bao hilo kwa shuti la wastani la mguu wa kulia baada ya kumpora mpira beki wa Namungo Derick Mukombozi, ambaye alizembea kuondosha hatari langoni mwake alipotaka kujaribu kumpiga chenga mshambuliaji huyo wa Yanga.
Ikionekana kutotosheka na mabao hayo mawili, Yanga ambayo sasa imefikisha mabao 42 iliendelea kulisakama kama nyuki lango la Namungo FC na ikafanikiwa kupata bao la tatu kupitia kwa Aziz Ki ambaye alimalizia kwa shuti la mguu wa kushoto pasi ya Yao Attohoula na kufanya ubao usome 3-0.
Bao hilo lilikuwa la 11 kwa Aziz Ki kwenye Ligi Kuu msimu huu, moja nyuma ya kinara Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye hadi sasa amepachika mabao 12 huku Yao akifikisha pasi ya saba za mabao, moja nyuma ya kinara Kipre Junior ambaye amepiga pasi za mwisho nane.
Pamoja na Namungo kuruhusu mabao hayo matatu ya harakaharaka, haikuonekana kukata tamaa na mara kadhaa ilijaribu kuliweka matatani lango la wapinzani wao lakini safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa makini kuondosha hatari chache zilizoelekezwa kwake.
Hata hivyo, dakika ya 71, Namungo FC ilipata bao la kujifariji ambalo lilikuwa la kujifunga la beki wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Baka' alipokuwa katika harakati za kuokoa krosi ya Emannuel Charles ikiwa ni bao la tisa Yanga inaruhusu msimu huu.
Katika kipindi hicho cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji lakini ilikuwa ni Yanga ambayo wachezaji wake walioingia walifanikiwa kulinda ushindi.
Yanga ambayo ilikuwa uwanjani bila mastaa wake Pacome Zouazoa, Djigui Diarra, Khalid Aucho, Joseph Guede, Kennedy Musonda na Joyce Lomarisa iliwatoa Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya na Augustine Okrah ambao nafasi zao zilichukuliwa na Jonas Mkude, Shekhan Ibrahim na Bakari Mwamnyeto wakati Namungo iliwapumzisha Meddie Kagere, Hamis Nyenye, Pius Buswita na Jacob Massawe ambapo iliwaingiza James Mwashinga, Hashim Manyanya, Hamad Majimengi na Kelvin Sabato.