Prime
Yanga mtego upo hapa!

Yanga inatarajiwa kushuka uwanjani kesho Jumamosi katika mchezo ulioshikilia hatma ya kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo na ikichemsha kwa kutoka sare ya kufungwa maana yake itaondolewa michuano ya CAF na kusalia mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Yanga itavaana na MC Alger katika mchezo wa mwisho wa Kundi A wa michuano hiyo ya CAF ukiwa ni kutafuta timu moja itakayoungana na Al Hilal iliyotangulia mapema robo fainali kutoka kundi hilo.
Yanga ipo nafasi ya tatu kundini ikiwa na pointi saba, huku MC Alger ipo ya pili na pointi nane kila moja ikicheza mechi nne, ilihali Al Hilal yenyewe ina pointi 10 na itamalizana na TP Mazembe yenye alama mbili.
Ushindi pekee katika mchezo huu ndio utaipa Yanga nafasi ya kufuzu robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo kwani itafikisha pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wao hao, ambao kwao sare inatosha kuwapa nafasi hiyo adhimu.
Hata hivyo, Yanga inatakiwa kuchukua tahadhari kubwa kutokana na tabia za timu nyingi za Kanda ya Kaskazini zinapokuwa zinatakiwa kupata sare ili kufuzu kwa hatua inayofuata.
Wachezaji wa Yanga wanatakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa wanaepuka mtengo wa wageni wao waliowasili jana alfajiri hapa nchini, wakielezwa kuwa wamebeba kila kitu, vikiwemo vyakula vyao na maji.
Kulalamika kwa waamuzi
Hii ni moja ya mbinu ambazo wamekuwa wakiitumia MC Alger katika mchezo ambao wanahitaji sare au wakiwa tayari wanaongoza kwenye mchezo husika.
Hutumia nguvu kubwa kulalamika kwa mwamuzi kila tukio linapotokea, na wanaweza kumzonga wakiwa wachezaji wanne au watano kwa wakati mmoja, hali hii wamekuwa wakiitumia kama mbinu ya kupoteza muda kwa kuwa wakati wanazozana na mwamuzi wanaweza kutumia dakika moja au sekunde 45 kwa tukio moja.
Wakati mwingine hali hii wanaifanya wakati ambao wanaona kuwa Yanga wanakwenda kushambulia, Yanga wanatakiwa kuhakikisha wanamfuata mwamuzi haraka na kumweleza kuhusu janja ya jamaa hawa kwani kumuacha kuna maanisha kuwa watarudi tuki hilo mara kadhaa.
Kujiangusha
Hii ni akili nyingine ambayo wamekuwa wakiitumia sana kwenye michezo yao ambao maamuzi yanakuwa mkononi mwao.
Ni rahisi kwa wachezaji wao kujiangusha hata wawili kwa wakati mmoja na madaktari wao huchelewa kuingia uwanjani makusudi na hata wakiingia wanakuwa wachache ambao huenda kwa mchezaji mmoja na baada ya kumaliza ndiyo huelekea kwa mwingine, hali hii wanaweza kuitumia sana dakika 20 za mwisho za mchezo.
Pamoja na kuwasaidia kupoteza muda pia imekuwa ikipunguza kasi ya mashambulizi na kuwapa mwanya wa kupumzika. Yanga wanachotakiwa kama hali hii ikitokea wanatakiwa kuwa watumwa, ni vyema madaktari wao kutoa msaada kwa mchezaji mmoja kwa kuwa kanuni hazikatazi.
Lakini pia ni vyema, wachezaji wa Yanga wakiona jambo hilo wamfuate mwamuzi na kumlalamikia kuhusu tukio hilo.
Kipa kuvua glovu
Mara nyingi mbinu yao kubwa ambao wamekuwa wakiitumia ni kipa kuvua gloves kila anapodanganya kuwa ameumia ili kupoteza muda wakati wa kuvaa, hali hii imekuwa ikimsaidia kupoteza muda kwa zaidi ya dakika moja wakati wa kutibiwa na kuvaa.
Lakini pia mara nyingi atamwita mchezaji mwezake na kumuomba amfunge viatu ambavyo atakuwa amevifungua mwenyewe akiwa amevua gloves.
Wakati wa kupiga mpira mbele makipa wa timu hizo husogea hadi kwenye nguzo ya goli taratibu na kuigonga na kisigino mara mbili au tatu, jambo pekee ambalo linaweza kuwaokoa Yanga na karaha hii ni kipa huyo kuwa na kadi ya njano ya mapema kitu ambacho kitamfanya aongope kupewa kadi nyekundu.
Mipira miwili uwanjani
Kuna wakati watakuwa wanatumia mbinu ya kuingiza mipira miwili uwanjani, mmoja aidha mashariki na mwingine Magharibi ili tu kuzua mechi isiendelee hadi mmoja utakapotolewa nje jambo ambalo linaweza kuwazuia Yanga kuharakisha jambo lao kama walikuwa wanashambulia kwa kasi au kutumia njia hiyo kupoteza muda.
Mabadiliko dakika za mwishoni
Timu hizi huweka wachezaji wawili au wakati nje ambao huwafanyia mabadiliko mwishoni mwa mchezo kama bado wana faida ya kile walichokuwa wanakitaka. Mara nyingi wachezaji ambao wanatolewa kwa wakati ule huwa mbali sana na sehemu ambao wanatakiwa kutokea, hukaa katikati ya uwanjani ambao kwenda Mashariki na Magharibi ni mbali, hukaa mwisho kabisa ya uwanjani na wanapoitwa hulazimisha kupitia katikati ya uwanjani.
Hapa akili inatakiwa kutumika, mchezaji wa Yanga akimsukuma ili aende nje haraka atajiangusha na kupoteza muda zaidi au kumtengenezea kadi, jambo pekee ni kukimbia kwa mwamuzi na kumshinikiza amwarakishe mchezaji huyo kutoka nje haraka.
Ili kuepuka haya, Yanga inatakiwa kutafuta ushindi wa mapema ili kuwafanya wapinzani wao kurudi uwanjani na kucheza kwa nguvu kubwa.