Prime
Yanga msako umeanza

Dar es Salaam. Mabosi wa Yanga wanaendelea na vikao vya ndani na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Miguel Angel Gamondi ili kujadili ishu za usajiri ila msako mkubwa ukiwa ni kwa straika wa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Fiston Mayele wanayemuuza nje ya nchi.
Mayele aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara sambamba na Saido Ntibazonkiza wa Simba kila mmoja akifunga mabao 17, huku akifunga mengine saba na kuwa kinara wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, amemalizana na Yanga tangu Jumatatu ya wiki hii ili kuondoka klabuni.
Straika huyo aliyefunga jumla ya mabao 33 ya Ligi Kuu kwa misimu miwili aliyoitumikia Yanga, alikuwa akishinikiza kuondoka licha ya kusaliwa na mkataba wa mwaka mmoja kutokana na kuwa na ofa ya donge nono kutoka Pyramids ya Misri na Al Qadisiyah ya Saudi Arabia anayoichezea Simon Msuva na kuwafanya mabosi wa Yanga wasiwe na namna ila kumruhusu aondoke tu.
Kutokana na kuondoka kwa Mayele, kumewafanya mabosi wa Yanga kuanza kukuna kichwa na kufikiria mtu wa kuziba pengo hilo, kukiwa na majina zaidi ya manne mezani mwao, huku wakimsikilizia zaidi Kocha Gamondi aliyeshikilia mpini kwa sasa klabuni hapo baada ya Nasreddine Nabi aliyemaliza mkataba na kuondoka.
"Kuna sapraizi inakuja ya usajili wa straika mpya wa kuchukua nafasi ya Mayele, ila imekuwa ngumu kwa sasa kuyajua majina, kwani vikao vinaendelea na inasubiriwa kujua straika huyo Mkongo atatua wapi na klabu itanufaika vipi na fedha za mauzo yake kwa mchezaji mpya atakayekuja," kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga.
Awali Yanga ilikuwa ikimtaka Makabi Lilepo kutoka Al Hilal ya Sudan, lakini dau kubwa liliwarudisha nyuma mabosi wa Yanga na wakaamua kukomaa kushusha wachezaji watatu wa kigeni akiwamo mabeki wa kati Gift Fred na Kouassi Yao na winga Maxi Mpia Nzengeli na wazawa Nickson Kibabage na Jonas Mkude.
"Ndani ya wiki ijayo kila kitu kinaweza kuwa wazi, lakini kwa sasa ukweli ni kwamba mabosi wapo bize kupitia majina ya wachezaji wanaoweza kuja kuendeleza pale alipoishia Mayele," kilisema chanzo hicho.
Yanga inaendelea kujifua kwa sasa kwenye kambi iliyopo kijiji cha Avic Town, Kigamboni chini ya Gamondi raia kutoka Argentina akisaidiana na Moussa N'Daw kutoka Senegal.