Yanga ishindwe yenyewe Caf

Mshambuliaji mpya wa Yanga, Prince Dube akishangilia bao lake la kwanza akiwa na jezi ya Wananchi dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini katika mechi ya kirafiki. Picha na Yanga
Muktasari:
- Vital'O, inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kukutana na Yanga, imeomba kutumia Uwanja wa Azam Complex, baada ya uwanja wao wa Intwali, Bujumbura kutopitishwa na Caf.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutoa orodha ya viwanja vilivyoruhusiwa kutumika kwa michezo ya mashindano yaliyo chini yao kwa msimu wa 2024-2025 ambayo ni Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, Klabu ya Vital'O kutoka Burundi imeomba kuutumia Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kwa mechi zao za nyumbani.
Vital'O inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kuanza na Yanga, imechukua uamuzi huo baada ya uwanja wao wa nyumbani wa Intwali uliopo Bujumbura, Burundi kutopitishwa na Caf.
Kitendo cha Vital'O kukubaliwa kuutumia Uwanja wa Azam Complex, kinaifanya Yanga sasa kutosafiri kwenda nje ya Dar es Salaam kucheza dhidi ya wapinzani wao hao katika mchezo wa hatua ya awali wa michuano hiyo.
Yanga awali ilitakiwa icheze ugenini Agosti 17 mwaka huu kwa kuifuata Vital'O katika mechi ya mkondo wa kwanza raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini sasa itasalia Dar es Salaam kucheza mechi zote mbili kama ilivyokuwa msimu uliopita ilipovaana na Asas ya Djibouti na kushinda jumla ya mabao 7-1.
Mchezo wa pili Yanga itakuwa mwenyeji dhidi ya Vital'O, Agosti 24 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Timu itakayoshinda kwa matokeo ya jumla itatinga hatua inayofuata na kucheza dhidi ya mshindi kati ya CBE ya Ethiopia na SC Villa kutoka Uganda kuwania kutinga makundi.
Meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Amir Juma, ameliambia Mwananchi kwamba, Vital'O ni kati ya timu tano zilizoomba kuutumia uwanja huo kwa mechi za kimataifa msimu wa 2024-2025.
"Tumepokea maombi ya Vital'O na tumeshawajibu kwamba tumewakubalia na kwamba mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Yanga itafanyika hapa Azam Complex. Mbali na Vital'O pia nyingine zilizoomba ni Rukinzo ya Burundi, Horseed ya Somalia zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika," amesema.
Alizitaja nyingine ni As Arta Solar 7 ya Djibouti, Dekadaha ya Somalia zitakazokutana katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisema safari hii hadi sasa Yanga haijaomba kuutumia uwanja huo.
Amir alisema sio Yanga tu, bali hata timu nyingine za ndani Simba na Coastal Union nazo hazijaomba hadi sasa ingawa kwa mujibu wa taarifa kutoka Klabu ya Coastal ni kwamba huenda ikahamia hapo kwa mechi hizo za Caf na zile za Ligi Kuu Bara itatumia Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam kwani Uwanja wa Mkwakwani, Tanga upo katika ukarabati.
"Timu ya ndani hapa itakayotumia uwanja huu ni Azam FC ambao ni wenyeji, lakini klabu zingine bado hatujapokea maombi yao, labda tusubiri kwa kuwa klabu kama Simba wao hawaanzii hatua hii, labda huko mbele wataleta maombi yao," amesema Amir.
Wakati huohuo, kikosi cha Yanga kilichopo Afrika Kusini katika ziara yao ya pre-season, jana kilifika Johannesburg kikitokea Mpumalanga tayari kwa mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs utakaochezwa Julai 28 mwaka huu kwenye Kombe la Toyota. Ikiwa Afrika Kusini, Yanga tayari imecheza mechi mbili dhidi ya FC Augsburg na kufungwa mabao 2-1, kisha ikashinda 1-0 dhidi ya TS Galaxy.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amezungumzia maendeleo ya kikosi chao akisema: "Tunafurahishwa na kiwango cha timu yetu na muunganiko unaoendelea kupatikana, Yanga tumesajili wachezaji wapya na hakuna mambo ya kupeana muda. Yanga inasajili mchezaji mpya anaingia kwenye timu na anatupa matokeo."
Katika mechi hizo mbili, imeshuhudiwa washambuliaji wapya wa Yanga, Jean Baleke akifunga dhidi ya Augsburg na Prince Dube akitupia mbele ya TS Galaxy.