Wolves ilivyoshushwa daraja Ligi Kuu England
Baadhi ya wachezaji wa Wolverhampton wakionekana kusikitika kutokana na matokeo mabaya waliokuwa wakipata katika mechi za mashindano Englanda. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kushuka daraja kwa Wolves kunahitimisha safari yao ya misimu nane mfululizo katika Ligi Kuu England, na sasa watashiriki Championship kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2017/18.
Wolverhampton ni rasmi sasa imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu England (EPL) hadi Championship kufuatia matokeo ya sare tasa katika mechi ya West Ham na Crystal Palace iliyochezwa jana Jumatatu, Aprili 20, 2026.
Matokeo hayo yameifanya West Ham kufikisha idadi ya pointi 33, huku Wolves ikiwa na pointi 17 pekee, hali inayomaanisha kuwa timu hiyo haiwezi tena kuwafikia wapinzani wao wakiwa wamebakiza michezo mitano kabla ya msimu kumalizika.
Wolves walianza msimu chini ya kocha Vítor Pereira, ambaye alifutwa kazi Novemba mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Rob Edwards, kocha wa zamani wa Luton Town na Middlesbrough.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuleta mafanikio yaliyotarajiwa, kwani Wolves walipata ushindi wao wa kwanza Januari na tangu hapo wameshinda michezo miwili dhidi ya Aston Villa na Liverpool.
Kushuka daraja kwa Wolves kunahitimisha safari yao ya misimu nane mfululizo katika Ligi Kuu England, na sasa watashiriki Championship kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2017/18.
Akizungumza baada ya kuthibitisha kushuka daraja, kiongozi wa muda wa klabu hiyo, Nathan Shi, amesema hayo ni matokeo yaliyowaumiza.
“Ni wakati mgumu kwa kila anayehusiana na Wolves. Haya ni matokeo yanayoumiza, lakini tayari tumeanza maandalizi ya kurekebisha hali hii kwa umakini na uthabiti,” amesema Shi.
Aliongeza kuwa klabu hiyo inaelewa maeneo ya kuboresha na sasa inalenga kujenga upya kikosi imara kitakachorejesha imani ya mashabiki.
“Mmetuunga mkono nyumbani na ugenini, na hatulipuuzii hilo. Mnastahili pongezi zaidi, na hilo ndilo litakalotuongoza katika hatua zinazofuata,” amesisitiza.