Wanajeshi vitani mashindano ya ndondi Taifa

Muktasari:
Mashindano hayo yataanza saa nane mchana yakitanguliwa na zoezi la kupima uzito na afya litakalofanyika kwa saa tatu kuanzia saa 12 asubuhi kwenye viwanja vya Tanganyika Pakers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Timu za vikosi vya Majeshi za Ngome, JKT, Magereza na Polisi zinaingia vitani sambamba na zile za kiraia kusaka bingwa wa ndondi taifa leo.
Mashindano hayo yataanza saa nane mchana yakitanguliwa na zoezi la kupima uzito na afya litakalofanyika kwa saa tatu kuanzia saa 12 asubuhi kwenye viwanja vya Tanganyika Pakers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga aliliambia gazeti hili jana kwamba, timu za Taasisi za majeshi ya Ulinzi na Usalama zimepewa hadhi ya mikoa katika mashindano hayo sambamba na zile za manispaa za Jiji la Dar es Salaam.
“Tayari, timu kutoka baadhi ya mikoa zimewasili jijini Dar es Salaam na nyingine zinatarajiwa kuingia leo (jana) jioni,” alisema Mashaga na kuongeza:
“Kesho (leo) asubuhi mabondia wote watapima uzito na afya, zoezi litakaloanza saa 12.00 asubuhi, kisha itachezeshwa droo ya nani atazichapa na nani na mashindano kufunguliwa rasmi saa 8.00 mchana.”
Katika hatua nyingine, mkutano Mkuu wa BFT uliokuwa ufanyike jana umekwama kutokana na idadi ya wajumbe kutotimia.
“Mkutano huu utapangiwa siku nyingine kwani idadi haikutimia na sasa tunaelekea katika maandalizi ya mashindano ya Taifa ya ndondi,” alisema Mashaga.