Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita yamvurugia Msuva Taifa Stars, Morice achukua nafasi

Muktasari:

  • Taifa Stars imepangwa kucheza dhidi ya timu ya taifa ya Liechtenstein tarehe 26 Machi katika Uwanja wa Kigali Pele. Mechi hiyo ni sehemu ya mashindano ya FIFA Series yanayolenga kuzipa timu za taifa nafasi ya kucheza na wapinzani kutoka mabara tofauti na kuongeza ushindani wa kimataifa.

Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imepata pigo kabla ya mechi zijazo za mashindano ya FIFA Series baada ya mshambuliaji Simon Msuva kuondolewa kikosini kutokana na matatizo ya usafiri yanayohusiana na mgogoro unaoendelea unaohusisha Marekani na Israel.

Msuva, anayechezea Al-Talaba SC inayoshiriki Ligi Kuu Iraq, ameshindwa kujiunga na kikosi hicho, jambo lililomlazimu kocha mkuu Miguel Gamondi kufanya mabadiliko ya ghafla kwenye safu ya ushambuliaji.

Gamondi amethibitisha kuwa juhudi za kumpata mshambuliaji huyo hazikufanikiwa, hivyo kuamua kumchukua Morice Abraham wa Simba SC kama mbadala wake.

“Tulifanya kila liwezekanalo kuhakikisha Msuva yupo kwenye kikosi, lakini haikuwezekana kutokana na hali ilivyo sasa. Tumemjumuisha Morice Abraham ili kuimarisha timu,” amesema Gamondi.

Licha ya changamoto hiyo, maandalizi ya mashindano yanaendelea, ambapo tayari timu imefanya mazoezi ya kwanza jijini Dar es Salaam kabla ya kuondoka kuelekea Kigali, Rwanda leo, Jumanne, Machi 24, 2026.

Gamondi amebainisha kuwa mazoezi yaliyosalia yatafanyika Rwanda.

Hata hivyo, kikosi bado kinawasubiri wachezaji wanaocheza nje ya nchi ambao wanatarajiwa kujiunga moja kwa moja na timu hiyo Kigali. Hawa ni pamoja na Kelvin John wa Aalborg (Denmark), Haji Mnoga wa Salford City, na Tarryn Allarakhia wa Rochdale zote zikiwa za England.

“Tumeanza mazoezi kwa siku moja na tutaendelea na maandalizi Kigali. Tunatarajia ushindani mkali, lakini wachezaji wako tayari,” ameongeza Gamondi.

Taifa Stars imepangwa kucheza dhidi ya timu ya taifa ya Liechtenstein tarehe 26 Machi katika Uwanja wa Kigali Pele. Mechi hiyo ni sehemu ya mashindano ya FIFA Series yanayolenga kuzipa timu za taifa nafasi ya kucheza na wapinzani kutoka mabara tofauti na kuongeza ushindani wa kimataifa.

Mchezo huo una umuhimu mkubwa kwani utaamua hatima ya Kundi B, ambapo mshindi atatinga fainali itakayochezwa Machi 29. Kwa Tanzania, huu ni fursa adimu kupima uwezo dhidi ya timu ya Ulaya, jambo ambalo kwa kawaida hutokea mara chache nje ya mashindano makubwa.

Mbali na matokeo ya haraka, mechi hiyo itakuwa jukwaa muhimu kwa benchi la ufundi kutathmini mifumo ya kiufundi, kupima maendeleo ya kikosi na kuona jinsi wachezaji wanavyoweza kuendana na mitindo tofauti ya kiuchezaji.

Kukabiliana na timu za Ulaya kutaiweka Taifa Stars kwenye changamoto muhimu kama kasi ya mchezo, nidhamu ya nafasi na uwezo wa kufanya maamuzi chini ya presha—vipengele muhimu kwa maendeleo katika ngazi ya kimataifa.

Pia ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazofanyika Kenya, Tanzania na Uganda.