Utamu wa Ulaya kuendelea tena leo

Muktasari:
- Kubwa ni mabadiliko ya michuano hiyo ya msimu huu, kuna timu 36 zitachuana kuwania ubingwa huo wa Ulaya na kila timu italazimika kucheza mechi nane kabla ya kutambua hatima yao ya kuingia hatua ya mtoano.
England. Ule utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya utaendelea tena usiku wa leo Jumatano na kesho Alhamisi kwa vigogo kibao kuonyeshana ubabe kwenye mchakamchaka wa kuwania ubingwa wa taji hilo kwa msimu huu wa 2024-25.
Kubwa ni mabadiliko ya michuano hiyo ya msimu huu, kuna timu 36 zitachuana kuwania ubingwa huo wa Ulaya na kila timu italazimika kucheza mechi nane kabla ya kutambua hatima yao ya kuingia hatua ya mtoano.
Kuna timu kadhaa zitaonekana kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza msimu huu, lakini macho ya wengi hii leo yataelekezwa huko Etihad, wakati wababe wanaopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa, Manchester City itakapokuwa na kibarua kizito cha kuwakabili Inter Milan.
Mashabiki wa michuano hiyo ya ubingwa wa Ulaya kwa ngazi za klabu wanatarajia kuona mechi ya kibabe kabisa kutokana na timu zote kuwa na uzoefu mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Itakuwaje hapo Etihad?
Man City na Inter Milan zilikutana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2022/23 na chama la Pep Guardiola liliibuka na ushindi, hivyo mchezo huo wa usiku wa leo utakuwa wa visasi. Patachimbika.
Kasheshe jingine la michuano hiyo litakuwa huko Parc des Princes, wakati wenyeji Paris Saint-Germain itakapokuwa wenyeji kuikaribisha Girona. Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa PSG kucheza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza bila ya huduma ya supastaa wao Kylian Mbappe, ambaye alitimkia zake huko Real Madrid kwa uhamisho wa bure kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi mwaka huu.
Mechi nyingine za usiku wa leo na Bologna itakipiga na Shakhtar Donetsk, wakati Sparta Prague itakuwa nyumbani kucheza na RB Salzburg, huku Celtic ikiwa kwao Scotland kucheza na Slovan Bratislava, wakati Wabelgiji Club Brugge itakuwa na kazi nzito ya kukipiga na Borussia Dortmund, iliyocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Kesho, Alhamisi shughuli pevu itakuwa huko Italia, wakati Atalanta, mabingwa wa Europa League wa msimu uliopita watakapokuwa na kibarua kizito mbele ya Arsenal. Kipute hicho kitapigwa kwenye Uwanja wa Gewiss, huku Arsenal ikiwa na mzuka baada ya kutoka kuwachapa mahasimu wao Tottenham Hotspur bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.
Mechi nyingine ya kibabe sana itakayopigwa usiku wa kesho, Atletico Madrid ya Diego Simeone itakuwa na kazi nzito mbele ya Wajerumani, RB Leipzig, huko AS Monaco itakuwa Ufaransa kumpa kibarua cha kwanza cha Ulaya kocha Hansi Flick huko kwenye kikosi cha Barcelona. Mjerumani, Flick ameanza maisha yake vyema huko Barcelona akishinda mechi zote alizoiongoza timu hiyo kwenye La Liga, lakini usiku huo wa kesho itakuwa zamu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Atafanya nini?
Mechi nyingine za mikikimikiki hiyo, Feyenoord itakipiga na Bayer Leverkusen, wababe wa Xabi Alonso waliocheza bila ya kupoteza mechi kwa msimu mzima uliopita kwenye Bundesliga, huku Benfica itaanzia ugenini kampeni yao ya msimu huu kwa kukipiga na FK Crvena Zvezda huku Brest itamalizana na Sturm Graz. Kwenye hatua hii ya kwanza kwenye mfumo mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuna kurudiana.
Vikosi vinavyotarajiwa huko Etihad;
Man City (3-2-4-1): Ederson, Manuel Akanji, Ruben Dias, Josko Gvardiol, Rico Lewis, Mateo Kovacic, Jérémy Doku, Bernardo Silva, Kevin De Bruyne, Jack Grealish, Erling Haaland.
Inter Milan (3-5-2): Yann Sommer, Benjamin Pavard, Francesco Acerbi, Alessandro Bastoni, Matteo Darmian, Nicolò Barella, Hakan Calhanoglu, Henrikh Mkhitaryan, Federico Dimarco, Marcus Thuram, Lautaro Javier Martinez.