United moto wake hatari, Chelsea yashinda

Muktasari:
- Mambo kwa upande wa Tottenham, hayakuwa mazuri kwa leo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Fulham.
Manchester United imeonekana kurudisha makali yake baada ya kuichapa Everton mabao 4-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
Huu ulikuwa mchezo wa pili kwa kocha mpya wa United, Ruben Amorim ambaye alianza mechi yake ya kwanza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya vibonde Ipswich.
Katika mchezo huu, ambao United walionekana kucheza kwa kasi ya juu walifanikiwa kujipatia mabao yao kupitia kwa Marcus Rashford aliyefunga mawili dakika ya 34 na 46, huku mengine yakiwekwa kimiani na Joshua Zirkzee katika dakika ya 41 na 64.
Matokeo hayo yameifanya Manchester United kufufua matumaini upya baada ya kupanda hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo ikiwa na pointi 19 baada ya michezo 13.
Mechi nyingine imeshuhudia Chelsea ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Aston Villa na kuendelea kuongeza presha kwa Liverpool, Arsenal na Man City kwenye kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Nicolaus Jackson, Cole Palmer na Enzo Fernandes na kuendelea kujikita nafasi ya tatu wakiwa na pointi 25 baada ya michezo 13.
Mambo kwa upande wa Tottenham, hayakuwa mazuri kwa leo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Fulham.
Spurs ilianza kufunga katika dakika ya 54 kupitia kwa Brennan Johnson huku Fulham ikisawazisha dakika ya Tonn Cairnny.
Spurs sasa ipo katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 20, huku Fulham ikiwa nafasi ya kumi na pointi 19