Try Again: Lengo limetimia Simba, ila bado!

Wachezaji wa Simba wakishangilia bao dhidi ya Horoya katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Picha na Loveness Bernard.

Muktasari:

  • Simba imetinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Horoya ya Guinea mabao 7-0 ikifikisha pointi tisa nyuma ya Raja Casablanca iliyokusanya pointi 13 ikiongoza Kundi C.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Salum Abdallah 'Try Again' amesema kutinga kwa timu hiyo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Agfrika ni moja ya malengo yao na kusisitiza wanaelekea kufikia hatua waliyokuwa wanaitamani miaka mingi yaani nusu fainali.

Simba imetinga robo fainali kibabe baada ya kuifunga Horoya ya Guinea kwa mabao 7-0 ikifikisha pointi tisa ikiwa nyuma ya Raja Casablanca iliyokusanya pointi 13 ikiongoza Kundi C, Horoya ikiwa ya tatu na pointi nne na Vipers inaburuza mkia na pointi mbili kila timu ikicheza mechi tano.

Akizungumza na Mwanaspoti, Try Again alisema malengo  ya klabu hiyo yalikuwa ni kuhakikisha wanaitengeneza Simba kuwa tishio ambayo inaweza kupambana na timu zingine kubwa zaidi Afrika sehemu ambayo ndio wanaelekea sasa.

"Tulikuwa kwenye mtihani mkubwa wa kuhakikisha tunaiona Simba ikitinga hatua ya robo fainali hili limefanikiwa na tulibezwa sana kwamba tuna kikosi kibovu, lakini safari inaendelea sasa na huko tuendako pia tuna nafasi ya kufanya vizuri pamoja na wengi kuzungumza mambo mengi;

"Tutawajibu kwa vitendo mpira unachezwa uwanjani na sio midomoni mwa watu kama ingekuwa hivyo kwa kuzungumzwa Simba inafungwa tusingeweza kufika hapa tulipo sasa tusubiri dakika nyingine tutakazozipata matokeo ndio yataamuliwa na tupo tayari kupambana na yeyote." alisema Try Again.

Alisema licha ya kupenya robo, lakini mikakati yao ni kuifanya Simba kuwa kwenye ushindani na timu kama Raja Casablanca iliyotuonyesha ubora na tumejifunza kitu kutoka kwao na vile wana mchezo dhidi yao kukamilisha ratiba tutaendelea kwenda kupambana na kujifunza ili kujipanga kwa robo.

“Tunataka kuwa na timu bora na ya ushindani yenye kutamba Afrika na nje ya mipaka ya bara hili. Hapa tulipo ni mwanzo tena wa mbali sana katika kusuka klabu ambayo haitakuwa na mpinzani wa kushindana nayo,” alisema Try Again.

Alisema wanaheshimu timu ambazo wanaweza kukutana nazo lakini na wao wanaheshima kubwa kwenye mashindano hayo watajiandaa vyema kuhakikisha wanaonyesha ushindani na kufikia malengo ya kufikia hatua ya nusu fainali.

Simba itaifuata Raja ugenini mechi itakayopigwa Aprili 1, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kumalizia mchezo wa mwisho dhidi ya Raja Casablanca ambao waliwafunga mabao 3-0 nyumbani wanaweza kukutana na timu hizi hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Mamelodi, Esperance au Wydad Casablanca.