Trump apongeza FIFA kwa kupindua adhabu ya Balogun
Muktasari:
- Kwa kadi nyekundu aliyopewa asingweza kucheza mtanange ujao. Ni mfungaji mzuri wa mabao wa Marekani. Ubelgiji wapinga uamuzi huo.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameishukuru FIFA kwa kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, hatua iliyomfungulia njia ya kucheza mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ubelgiji.
Balogun alioneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya mwamuzi kupitia mfumo wa VAR katika ushindi wa Marekani wa mabao 2-0 dhidi ya Bosnia na Herzegovina, baada ya kumkanyaga mguu beki Tarik Muharemovic.
Kwa mujibu wa Kanuni za Nidhamu za FIFA, mchezaji anayepata kadi nyekundu ya moja kwa moja hufungiwa moja kwa moja mechi moja inayofuata, huku adhabu hiyo kwa kawaida isiyoweza kukatiwa rufaa na timu husika.
Hata hivyo, Kamati ya Nidhamu ya FIFA ilitangaza Jumapili kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 27 cha Kanuni za Nidhamu za FIFA, utekelezaji wa adhabu hiyo umesimamishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa majaribio.
FIFA ilifafanua kuwa ikiwa Balogun atafanya kosa jingine la aina na uzito unaofanana ndani ya kipindi hicho, adhabu hiyo itarejeshwa na kutekelezwa pamoja na adhabu yoyote atakayopata kutokana na kosa jipya.
Uamuzi huo unamruhusu Balogun kuendelea kuichezea Marekani katika mchezo muhimu dhidi ya Ubelgiji utakaochezwa Seattle.
Mshambuliaji huyo amekuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya Marekani katika Kombe la Dunia 2026, akiwa tayari amefunga mabao matatu, yakiwemo mawili katika ushindi wa mechi ya ufunguzi dhidi ya Paraguay.
Dakika chache baada ya FIFA kutangaza uamuzi huo, Trump aliandika kupitia mtandao wake wa Truth Social.
"Asante FIFA kwa kufanya jambo sahihi na kurekebisha dhuluma kubwa,” alisema Trump.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Marekani limesema linaunga mkono uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya FIFA.
"Sasa nguvu zetu zote zimeelekezwa katika mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Ubelgiji mjini Seattle, na tunatarajia kuendelea kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wetu," ilisema taarifa ya shirikisho hilo.
Ubelgiji walalamika
Lakini upande wa Ubelgiji umeonyesha kutoridhishwa na uamuzi huo.
Kocha wa timu hiyo, Rudi Garcia, alitoa kauli ya kejeli iliyoonyesha mshangao wake kuhusu hatua ya FIFA.
"Sikujua kwamba katika Kombe la Dunia, tarehe 5 Julai huwa kama Aprili Mosi, yaani Siku ya Wajinga (April Fool's Day)," alisema Garcia.
Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kama ukosoaji wa moja kwa moja dhidi ya uamuzi wa FIFA wa kusimamisha adhabu ambayo, kwa mujibu wa kanuni zake, ilipaswa kuanza kutumika mara moja.
Hatua ya FIFA imezua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka duniani, huku baadhi wakihoji iwapo matumizi ya Kifungu cha 27 yamekuwa ya haki na yenye kuzingatia usawa kwa timu zote zinazoshiriki mashindano hayo.
Wachambuzi kadhaa wameeleza kuwa uamuzi huo unakumbusha mijadala iliyowahi kuikumba FIFA wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa shirikisho hilo, Sepp Blatter.
Katika kipindi hicho, FIFA ilikosolewa mara kwa mara kwa maamuzi yaliyodaiwa kuwa hayakuwa wazi vya kutosha, pamoja na ukosefu wa uwazi katika baadhi ya maamuzi ya kinidhamu na kiutawala.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao