Timu ya taifa ya Kriketi imefuzu kucheza Kombe la Dunia

Muktasari:
- Hadi inamaliza kucheza mashindano hayo ya kufuzu Kombe la Dunia, timu ya Taifa ya Kriketi chini ya miaka 19 imeweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote mpaka imekuwa Bingwa.
Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Kriketi chini ya miaka 19 imefuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia baada ya kuishinda Sierra Leone katika mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia kwa Afrika ambayo yamefanyika nchini Nigeria.
Vijana hao walifanikiwa kuibuka mabingwa kwenye mashindano hayo baada ya kupata ushindi wa mikimbio 98 dhidi ya Sierra Leone na kujihakikishia kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia.

Mashindano hayo yalishirikisha nchi sita ikiwemo Tanzania, Namibia, Sierra Leone, Nigeria, Kenya na Uganda kwa ajili ya kufuzu fainali za kombe la Dunia litakalofanyika mwakani nchini Namibia na Zimbabwe.

Katika mshindano hayo yaliyofanyika Jijini Lagos, Nigeria, ilishuhudiwa timu hiyo ya vijana ya Tanzania ikimaliza mashindano bila kupoteza mchezo wowote.
Mchezo wa kwanza Tanzania iliibuka na ushindi wa mikimbio 73 dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya Uganda kabla ya kupata ushindi mwingine katika mechi ya pili ilipowafunga wenyeji Nigeria kwa mikimbio 122.

Kwenye mchezo wa tatu Tanzania iliendeleza ubabe kwenye mashindano baada ya kuifunga timu ya taifa ya vijana ya Namibia kwa kupata ushindi wa mikimbio 17.

Mchezo mwingine ilishuhudiwa vijana hao wakiifunga timu ya taifa ya Kenya kwa kupata ushindi wa mikimbio 54 kabla ya kutawazwa kuwa mabingwa baada ya kupata ushindi kwenye fainali ambapo iliifunga Sierra Leone kwa jumla ya mikimbio 98.