Taifa Stars yaporomoka viwango vya ubora FIFA
Muktasari:
- Taifa Stars haijapata ushindi chini ya Miguel Gamondi ambapo imepoteza mechi nne na kutoka sare mbili.
Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshuka kwa nafasi tatu katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vya mwezi huu.
Katika chati iliyowekwa hadharani leo, Ijumaa, Machi 27, 2026, Tanzania ipo nafasi ya 113 kutoka nafasi ya 110 ambayo ilikuwepo katika viwango vilivyopita vya mwezi Februari.
Kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Liechtenstein kwenye mashindano ya FIFA Series jana, kimeonekana kuchangia kuishusha Taifa Stars kwani wapinzani wao hao walikuwa katika nafasi ya 205 kabla ya mchezo huo.
Mara kwa mara, timu iliyo juu katika chati ya ubora ya FIFA ikipoteza dhidi ya timu ya chini, huanguka huku iliyo chini ikipanda.
Liechtenstein hata hivyo imebakia katika nafasi yake ya 205.
Kenya imepanda kwa nafasi moja hadi ya 112 wakati huo Uganda ikisalia katika nafasi ya 88 na Rwanda imepanda kwa nafasi moja kutoka ya 130 hadi nafasi ya 129.
Kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), iliyopanda kwa nafasi nyingi zaidi ni Sudan Kusini.
Sudan Kusini kwa sasa ipo nafasi ya 164 kutoka nafasi ya 169 ambayo ilikuwepo hapo awali.
Burundi ambayo ilikuwa nafasi ya 145, hivi sasa imepanda kwa nafasi mbili hadi ile ya 143.
Hispania inaendelea kuongoza chati ya Dunia mbele ya Ufaransa iliyopanda kwa nafasi moja hadi ya pili huku Argentina ikiporomoshwa kwa nafasi moja hadi nafasi ya Tatu.