Stars ni kufa au kupona Afcon 2025

Muktasari:
- Taifa Stars leo itacheza mchezo wa mwisho wa kufuzu Afcon 2025 dhidi ya Guinea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam utakaoanza saa 10:00 jioni.
Tunaitaka Afcon 2025. Hiyo ni kauli ya Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' akielezea namna alivyokiandaa kikosi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Guinea.
Taifa Stars leo itacheza mchezo wa mwisho wa kufuzu Afcon 2025 dhidi ya Guinea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam utakaoanza saa 10:00 jioni.
Ni mchezo wa lazima Stars kushinda ili kufuzu michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Morocco huku tumaini la Watanzania wengi ni uwepo wa nahodha, Mbwana Samatta na mshambuliaji Simon Msuva.
Samatta na Msuva ambao kwa namna moja ama nyingine walichangia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi iliyopita iliyofufua upya matumaini ya kufuzu, leo wanaangaliwa tena wakipewa jukumu zito la kuibeba timu hiyo.
Kwa mastaa waliopo Stars hivi sasa, Msuva ndiye kinara wa mabao wa jumla akifunga 23 katika michezo 93 tangu alipokitumikia kikosi hicho mwaka 2012, huku akibakisha mawili tu kuifikia rekodi ya Mrisho Ngassa aliyefunga 25, kwenye mechi 100 alizochezea kuanzia mwaka 2006 hadi 2015.
Samatta ndiye anayefuatia kwa ufungaji bora wa timu ya taifa baada ya kufunga mabao 22 katika michezo 82, tangu alipoanza kuichezea mwaka 2011.
USHINDI LAZIMA
Stars leo ni lazima ishinde ili ifuzu Afcon 2025 kutokana na kwamba katika Kundi H, tayari DR Congo imefuzu na pointi zake 12, Ethiopia yenye pointi moja, haina nafasi, huku kazi ikibaki kwa Guinea (9) na Stars (7).
Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema leo kazi ni moja tu kupata ushindi na kuipa nafasi timu hiyo kufuzu Afcon 2025.
"Tunajua ubora wa wapinzani wetu na sisi tunakwenda kwenye mchezo huo kwa lengo la kupata ushindi ingawa hautakuwa mchezo rahisi kutokana na wenzetu wakipata sare basi watafuzu moja kwa moja," alisema Morocco na kuongeza.
"Hakuna majeruhi hata mmoja kwenye kikosi, hali za wachezaji ni nzuri na wote wako na morali ya kuuendea mchezo huo muhimu kwetu."
Kipa wa Stars, Aishi Manula, akizungumza kwa niaba ya wachezaji, amesema: "Miaka ya nyuma tumekuwa tukisuasua kupata matokeo lakini hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko makubwa na kama wachezaji tuna matumaini makubwa juu ya mchezo huo muhimu na ushindi wa kesho ni maalumu kwa ndugu zetu waliopata ajali ya Kariakoo."
Stars ambayo tayari imeshashiriki michuano ya Afcon mara tatu 1980, 2019 na 2024, inaifukuzuia ya mwaka 2025 kabla ya 2027 kuwa mwenyeji. Kwa upande wa Guinea tayari imefuzu mara 14 huku mwaka 1976 ikimaliza nafasi ya pili baada ya Morocco kuwa mabingwa.
Katika mchezo wa kwanza, Stars iliifunga Guinea mabao 2-1 ugenini hivyo mchezo wa leo ni wa kisasi kwa Guinea lakini pia Stars kwao ni wa kuweka heshima.
Stars imekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika mechi tatu za mwisho nyumbani zikiwemo mbili za kufuzu Afcon dhidi ya Ethiopia iliyotoka sare kabla ya kufungwa 2-0 na DR Congo, mchezo wa leo ni kuondoa takwimu hizo mbaya.
Wakati Guinea yenyewe itaingia kwa lengo la kutopoteza mchezo ili kufuzu kwani kwao sare tu inawabeba.
Rekodi ya Guinea ugenini katika mechi tatu za mwisho zinaonyesha imeshinda mbili dhidi ya Ethiopia katika kufuzu Afcon na Algeria kuwania kufuzu Kombe la Dunia hali inayowapa matumaini makubwa kuelekea mchezo wa kesho.
GUIRASSY WAKUCHUNGWA
Straika wa Borussia Dortmund, Serhou Guirassy, amekuwa mchezaji muhimu akiibeba Guinea kutokana na kufunga mabao sita katika mechi tatu mfululizo zilizopita huku akiwa kinara wa jumla, kumbuka hakucheza mechi ya kwanza dhidi ya Stars.
Mshambuliaji huyo leo kazi itakuwa nzito kwa safu ya ulinzi ya Stars chini ya Ibrahim Bacca na Dickson Job kumzuia asifunge.
Kuhusu mkakati wa kumzuia straika huyo, kipa wa Stars, Aishi Manula, alisema wamemsoma vizuri Guirassy na kama safu ya ulinzi wana kazi ya kuikabili timu nzima.
"Tunafahamu ubora wa mshambuliaji huyo na ukiachana na hilo pia ana udhaifu wake hivyo tutajaribu kuutumia ili kupata bao na kocha ametupa mbinu za kukabiliana nao kwa namna watakavyokuja," alisema Manula.
Wakati Guinea ikitambia Guirassy, Stars inaye Feisal Salum ambaye anaongoza kwa mabao katika mechi hizo za kufuzu akiwa nayo mawili aliyofunga dhidi ya Guinea na Ethiopia.
Lakini pia, uwepo wa Msuva na Samatta unaongeza matumaini ya Stars kufuzu.
Huku Manula, Kule Camara
Makipa wawili wa Simba, Aishi Manula na Moussa Camara, watakuwa na vita yao kuzipambania timu zao kufuzu Afcon. Kwa vyovyote vile, mmoja atatoka uwanjani kifua mbele.
Manula ambaye mchezo uliopita ulikuwa wa kwanza kwake kucheza katika kufuzu Afcon 2025, aliondoka na clean sheet, huku Camara akiendeleza kile alichokianza huku naye akiondoka na clean sheet dhidi ya DR Congo.
Kwa sasa Camara ndiye kipa namba moja wa Simba akicheza mechi zote za kimashindano msimu huu, wakati Manula bado hajacheza mechi yoyote kutokana na kuwa nje muda mrefu akiuguza majeraha lakini sasa amepona.
Katika mchezo wa leo, kila mmoja atataka kuonyesha kitu kudhihirisha ubora wake.
Hakuna kiingilio
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema hakuna kiingilo kwenye mechi hiyo na lengo la kufanya hivyo ni kila Mtanzania kwenda kwa Mkapa kuishuhudia Stars ikicheza mchezo muhimu wa kufuzu.
"Kesho (leo) kila Mtanzania anapaswa kuja kwa Mkapa kuishuhudia Stars ambayo ina mchezo mgumu wa kufuzu uwepo wao uwanjani ni hamasa kubwa kwa wachezaji wetu kiwanjani na kwa watu elfu ishirini watakaowahi kuna zawadi kwa ajili yao," alisema Ndimbo.