Slot aipa matumaini Liverpool kuiondoa PSG
Muktasari:
- Liverpool itakuwa na kibarua cha kupindua matokeo ya mabao 2-0 iliyofungwa katika mechi ya kwanza.
Liverpool, England. Meneja wa Liverpool, Arne Slot, ametuma ujumbe wa kuhamasisha kikosi chake akiamini bado wana nafasi ya kufanya muujiza dhidi ya PSGkatika mchezo wa robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaopigwa katika Uwanja wa Anfield.
Liverpool wanaingia uwanjani wakiwa nyuma kwa mabao mawili kufuatia kupoteza mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Paris, ambapo walizidiwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, Slot anaamini kikosi chake kina uwezo wa kubadili matokeo hayo.
Akizungumza kabla ya mchezo huo, Slot amesema,
Kocha wa Liverpool, Arne Slot akizungumza na vyombo vya habari kuelekea katika mechi ya robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG. Picha na Mtandao
“ndiyo, tunaamini tunaweza kufanya mambo ya kipekee leo. Lakini tunapaswa kuwa wa kipekee sana kwa sababu tunacheza dhidi ya mabingwa wa Ulaya. Hilo linafanya kazi kuwa ngumu zaidi, lakini siyo jambo lisilowezekana.”
Uwanja wa Anfield umekuwa ukijulikana kwa matokeo ya kushangaza katika michuano hiyo, ikiwemo ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Barcelona mwaka 2019, ambapo Liverpool walipindua matokeo ya mabao matatu.
Nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk, amesisitiza umuhimu wa mashabiki katika mchezo huo, akisema wanaweza kuwa silaha kubwa kwa timu.
“Mashabiki watakuwa jambo muhimu sana, pamoja na kiwango chetu uwanjani. Tumewahi kushuhudia ushirikiano mkubwa kati ya mashabiki na wachezaji katika usiku kama huu,” amesema Van Dijk.
Kwa upande wake, kocha wa PSG, Luis Enrique, amekiri kuwa mchezo huo unaweza kuwa mgumu licha ya timu yake kuwa na faida ya mabao mawili.
Kocha wa PSG, Luis Enrique akizungumza na vyombo vya habari kuelekea katika mechi ya robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool. Picha na Mtandao
“Kuna mitego mingi katika mchezo huu, inaweza kuwa hatari. Watu wanaangalia tofauti ya wiki iliyopita, lakini bado utakuwa mchezo mgumu sana,” amesema Enrique.
Kiungo wa Liverpool, Dominik Szoboszlai, amesema wachezaji wote wako tayari kupambana hadi dakika ya mwisho ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
“Tutaingia kwa nguvu zote kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, hata kama itafika muda wa nyongeza. Tunaitaka sana nafasi hii, na tunajua Anfield itakuwa na mchango mkubwa,” amesema Szoboszlai.
Hata hivyo, Liverpool watalazimika kuboresha kiwango chao ikilinganishwa na mchezo wa kwanza ambapo hawakuwa na shuti hata moja lililolenga lango na walimiliki mpira kwa asilimia 26 pekee.
Slot amekumbusha kuwa timu yake imekuwa na rekodi nzuri nyumbani, akieleza kuwa Liverpool wamefunga angalau mabao mawili katika michezo 36 kati ya 50 iliyopita waliyocheza Anfield.
Kuna uwezekano wa kinda Rio Ngumoha kuanza baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi zilizopita, huku golikipa Alisson Becker akiendelea kukosekana kutokana na majeraha.
Mshindi wa matokeo ya jumla katika mchezo huo, atakutana na mshindi mwingine kati ya Real Madrid au Bayern Munich ambao watacheza kesho.