Prime
Sintofahamu kupewa uraia wa 'mchongo' wachezaji Singida

Muktasari:
- Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imetoa uraia kwa wachezaji watatu wa kigeni wa klabu ya Singida Black Stars (SBS), huku mjadala ukiibuka kuhusu uhalali wake kutokana na matakwa ya sheria yanavyoelekeza.
Dar es Salaam. Ni mshangao! Ndivyo unavyoweza kueleza kuhusu uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuwapa uraia wachezaji watatu wa klabu ya Singida Black Stars (SBS).
Watu wengi wanajiuliza kuhusu hatua hiyo na mazingira ya wachezaji hao kupewa uraia, huku wakionekana kutokuwa na muda mrefu tangu waingia nchini, jambo ambalo kwa mujibu wa wanasheria ni kinyume cha sheria za uhamiaji.
Wachezaji waliopewa uraia ni Emmanuel Keyekeh, ambaye ni raia wa Ghana, Josephat Bada wa Ivory Coast na Muhamed Camara kutoka Guinea.
Ukiacha suala hilo, umeibuka utata mwingine wa kisheria kuhusu madai ya Klabu ya Simba nayo kuwaombea uraia wachezaji wake wa kigeni tisa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amekiri ni kweli klabu yake imewasilisha barua ya maombi ya uraia kwa wachezaji wao tisa.
"Ni kweli tumeandika barua hiyo tukiomba utaratibu wa kufuatwa kwa wachezaji wetu tisa ambao, wanaomba uraia wa Tanzania," alisema Ahmed ambaye hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji wanaoombewa uraia kwa sasa.
Mwananchi limezungumza na baadhi ya mawakili ambao walionyesha kushangazwa huku wakisema mambo hayo yalipaswa kufanywa na wachezaji wenyewe, na sio klabu kama ambavyo Ahmed ameeleza.
Hata hivyo, kuhusu wachezaji wa SBS kupewa uraia, wanasheria hao wamesema ingawa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ana uamuzi wa mwisho katika kutoa uraia, lakini haimaanishi waziri akisigina sheria, uamuzi wake huo hauwezi kupingwa, kwani yapo mashauri ya kimahakama yanayotoa msimamo wa sheria.
Wakati wanasheria wakisema hayo, Idara ya Uhamiaji iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Januari 23, 2025 ilijitokeza hadharani kujibu hoja za wachangiaji mitandaoni, ikisema wachezaji hao waliomba na kupewa uraia kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya sheria ya uraia Tanzania.
“Kwa muktadha huo, Idara ya Uhamiaji inapenda kuutaarifu umma kuwa watajwa (wachezaji hao watatu wa SBS) ni raia wa Tanzania kwa Tajnisi,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI), Paul Mselle ambaye ni Msemaji Mkuu wa Idara hiyo ya Uhamiaji hapa Tanzania.
Leo Ijumaa, Januari 24, 2025, Mwananchi limewatafuta tena Uhamiaji kupata ufafanuzi zaidi wa suala hilo ambalo linaonekana kuibua mjadala wa kisheria ambapo Msemaji Mkuu wa Idara hiyo, Paul Mselle amesema ufafanuzi walikwisha kutoa katika taarifa kwa umma.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Mashungwa, Naibu Wake, Daniel Sillo hakupatikana, huku Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akisema hayupo kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo na kutaka atafutwe Kamishina Mkuu wa Uhamiaji, Jenerali Anna Makalala.
"Tulishawaeleza Uhamiaji walitolee ufafanuzi jambo hilo, hivyo muulize Kamishna wake (Makakala) atalijibu kwa ufasaha," amesema Msigwa. Hata hivyo, Makakala alipotafutwa kwenye simu yake iliita bila kupokelewa.
Sheria inasemaje?
Kwa mujibu wa sheria ya Uhamiaji Tanzania, sura ya 357, ili mgeni aweze kupewa uraia wa Tanzania, atapaswa kutimiza masharti yaliyowekwa na sheria ikiwamo awe anaelewa vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Kuna madai kuwa wachezaji wawili kati ya watatu wanazungumza lugha ya kifaransa pekee.
Masharti mengine ni lazima mwombaji awe na umri wa miaka 18 au zaidi na awe na uwezo wa kufanya uamuzi unaokubalika kwa mujibu wa sheria na awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miezi 12 mfululizo kabla ya kutuma maombi yake ya uraia.
Halikadhalika, sheria hiyo inataka katika muda wa miaka 10 kabla ya hiyo miezi 12, muombaji awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda usiopungua miaka saba, awe na tabia njema na awe amechangia katika ukuzaji uchumi, sayansi na teknolonia na utamaduni wa Tanzania.
Walichosema wanasheria
Akizungumzia uamuzi wa Serikali kuwapa uraia wachezaji, wakili Juma Nassoro amesema si jambo geni kwa wageni kupewa uraia kwa sababu ya mpira na kutolea mfano nchi ya Tunisia ilimpa uraia Mbrazil Jose Clayton mwaka 1998 na akaichezea Tunisia katika michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia Ufaransa.
Akiwachambua wachezaji hao wa SBL, wakili Nassoro amesema ni kweli Kayeke, ambaye ni raia wa Ghana ni fundi kweli kweli na ndiye mchezaji bora wa ligi ya ndani ya Ghana 2023/24 na tangu asajiliwe Julai 2024 ameonyesha uwezo mkubwa hadi ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi mara nne.
Kuhusu Bada, wakili huyo amesema SBS ilimsajili Julai 2024 kama kiungo na ilifanikiwa hivyo baada ya kuizidi ujanja Ismailia ya Misri huku kiungo Camara naye akisajiliwa Julai 2024 kuichezea klabu hiyo kama walivyo wachezaji wengine wa kigeni.
“Ukisoma Jedwali la Pili la sheria ya uraia ya Tanzania limeweka masharti kadhaa. Sharti moja linaeleza ni lazima muombaji awe ana ufahamu mzuri wa lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Swali ni kuwa Bada na Camara ambao wanazungumza kifaransa tu wamewezaje kukidhi kigezo hicho?” alihoji wakili huyo.
“Je, Waziri wa Mambo ya Ndani anafahamu kuwa kisheria ingawa sheria inaeleza kuwa. uamuzi wa waziri ni wa mwisho, haimaanishi kuwa Waziri akisigina sheria, uamuzi hauwezi kupingwa? Yapo maamuzi mengi ya Mahakama Kuu yaelezeayo msimamo huu kuntu wa sheria,” alisisitiza.
Kuhusu maombi ya Simba, wakili huyo alihoji inakuwaje uongozi ndio unatangaza kuwaombea uraia wachezaji badala ya kila mchezaji kuomba mwenyewe kwa hiyari yake.
Kwa upande wake, wakili Boniface Mwabukusi amesema, kimsingi sheria ya Uraia ya Mwaka 1995 imeweka bayana kigezo cha msingi cha mtu anayeomba uraia lazima awe ameishi Tanzania kwa kipindi kisicho pungua miaka 10 ingawa yapo mazingira maalumu mgeni anaweza kupewa uraia kabla ya hiyo miaka 10.
Aliyataja mazingira hayo kuwa ni kupewa uraia wa heshima na waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mtu huyo ni lazima awe amechangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii au kisayansi na anajulikana kimataifa kwa sifa nzuri au kwa mchango wa kipekee.
Mazingira mengine ambayo mtu anaweza kupewa uraia bila kusubiri miaka 10 ni pamoja na aliyepo katika ndoa katika kipindi kisichopungua miaka miwili, watoto wa mgeni aliye raia wa Tanzania, uraia kwa upendeleo maalum na wakimbizi ambao wanaweza kupewa uraia kabla ya kutimiza miaka 10.
“Ingawa sheria inataka muda wa miaka 10, kuna mazingira maalum kama niliyoyaainisha ambapo mgeni anaweza kupewa uraia kabla ya kutimiza muda huo. Hata hivyo, maamuzi yote ni kwa mamlaka ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye ana mamlaka ya mwisho juu ya maombi yote ya uraia,” alisema na kuongeza:
“Haya ni maoni yangu kwa ujumla lakini kila nikijaribu kuangalia hao wachezaji watatu wa Singida Black Star, sioni ni yupi kati yao anayeangukia katika exception (upekee) nilioeleza hapo juu. Niko najaribu kuendelea kulifanyia utafiti ili tuje na majibu yaliyo bayana,” alisisitiza wakili Mwabukusi.
Usajili wa Bada, Keyekeh na Camara
Mjadala wa wachezaji hawa kuwa na uhalali wa kupewa uraia unazidi kufuka moshi kutokana na kile kinachoonekana ni kukiukwa kwa sheria.
Mwnanchi linaamini kuwa Camara aliyesajiliwa na Singida Black Stars kutoka Hafia ya Guinea, ana miezi mitano na siku 20 tu alizoishi Tanzania kuanzia pale aliposajiliwa Julai 27, 2024 hadi siku ambayo dirisha dogo la usajili la Ligi Kuu lilipofungwa, Januari 15.
Kwa upande wa Keyekeh aliyesajiliwa kutokea Samartex ya Ghana na Arthur Bada aliyenaswa kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast, kila mmoja ana miezi mitano na siku 15 aliyotumikia Singida Black Stars, muda ambao ni mfupi kulinganisha na ule wa kisheria ambao anayeomba uraia anapaswa kutimiza kama masharti ya msingi.
Wachezaji hao kila mmoja alisajiliwa rasmi na SBS Agosti Mosi, 2024 kwa mujibu wa taarifa za usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara.
Pia, mpaka sasa hakuna hadhi mpya ya usajili kwa wachezaji hao licha ya kubadili uraia, kwani bado wanatumia hadhi ya usajili wa dirisha kubwa la usajili la kabla ya msimu kuanza wakitambulika kama wachezaji wa kigeni.
Juhudi za kumtafuta Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza kutolea ufafanuzi suala hilo ziligonga mwamba kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa.
Je wanaweza kuichezea Taifa Stars?
Oktoba 3, 2021 Serikali ya Tanzania ilitangaza kumpatia mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis Prosper uraia baada ya kuomba na kukidhi vigezo.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema kuwa Kibu alipewa uraia tangu Septemba 30, mwaka huo na kwamba, uamuzi huo ulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 (Rejeo la 2002), baada ya kupokea ombi lililopelekwa kwake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Kibu alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini amekuwepo nchini tangu mwaka 1998 wakati huo akiwa na miaka sita, baada ya wazazi wake kukimbia machafuko ya kisiasa nchini DRC. Kwa sasa Kibu amekuwa akiitwa kuitumikia timu ya Taifa, Taifa Stars.
Hata hivyo, licha ya sheria kumpa madaraka waziri ikiwemo kutajwa kwa baadhi ya sababu, suala la wachezaji hao watatu wa SBS kuichezea Taifa Stars itakuwa ndoto kwa sasa.
Mwananchi linatambua kuwa kutakuwa na ugumu kwa Bada (22), Keyekeh (27) na Damaro (22) kuichezea Taifa Stars kwa kuwa hawajatimiza vigezo vya kanuni za uthibitisho wa uraia zilizowekwa na Shirikisho la Mpira wa miguu Duniani (Fifa).
Ibara ya saba ya Kanuni za Fifa za uhalali wa mchezaji kuwakilisha timu za taifa, inataja vigezo vinne ambavyo vitamfanya mchezaji aliyebadilisha uraia aruhusiwe kuchezea timu ya taifa ya nchi husika.
1. Awe amezaliwa katika nchi husika
2. Baba au mama yake wa kibaiolojia awe amezaliwa katika nchi husika
3. Babu au bibi yake kibaiolojia awe amezaliwa katika nchi husika
4. Awe ameishi katika nchi husika, kama akiwa na umri chini ya miaka 10 angalau awe ameishi kwa miaka mitatu, kama ana umri wa miaka 10 hadi 18 angalau awe ameishi katika nchi husika angalau kwa miaka isiyopungua mitano, na kama ana umri wa zaidi ya miaka 18, awe ameishi katika nchi husika kwa muda usiopungua miaka mitano.