Simba yatoa wawili kikosi bora makundi CAF

Muktasari:
- CAF imetoa orodha ya wachezaji 11 bora, wanaounda kikosi cha timu moja, kutokana na mechi za hatua ya makundi ambapo Simba imetoa mastaa wake wawili waliofanya vizuri kwenye mechi sita za Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati mashabiki wa Simba wanachekelea ushindi wa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, Wekundu hao wakishinda kwa mabao 3-0 kuna taarifa itakayochagiza zaidi matokeo hayo ambayo Idara ya mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeitoa usiku huu.
CAF imetoa orodha ya wachezaji 11 bora, wanaounda kikosi cha timu moja, kutokana na mechi za hatua ya makundi ambapo Simba imetoa mastaa wake wawili waliofanya vizuri kwenye mechi sita za Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba imeungana na Zamalek, USM Alger, RS Berkane kwa kila timu kutoa wachezaji wawili kwenye kikosi hicho huku Al Masry na CS Constantine zikitoa mchezaji mmoja mmoja.

Mastaa wa Simba ambao wapo kwenye kikosi hicho ni nahodha na beki wa kushoto, Mohammed Hussein 'Tshabalala' na kiungo Jean Charles Ahoua ikiungana na Zamalek na RS Berkane ambazo nazo zimetoa idadi ya wachezaji wawili kila moja kwenye timu hiyo.
Kwenye ukuta huo Tshabalala amejumuishwa sambamba na kipa Munir Mohammed (RS Berkane), mabeki wengine wakiwa ni Saadi Radouani (USM Alger), Issoufou Dayo (Berkane) na Hossam Abdelmaguid wa Zamalek.
Eneo la kiungo wapo Ahmed Zizo (Zamalek), Brahim Dib (CS Constantine) na Ahoua huku safu ya mbele ikiwa na Seifeddine Jaziri (Zamalek), Ben Youssef (Al Masry) na Ismail Belkacemi (USM Alger).
Simba kesho itasubiri kujua itakutana na timu ipi kwenye hatua ya robo fainali ya droo ya mashindano hayo.