Simba yashusha kocha mwenye rekodi kali
Muktasari:
- Aliisaidia Black Princess kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake Under-20, Ufaransa 2018, Mashindano ya Michezo ya Afrika 2015, Congo Brazzaville.
Baada ya kusemekana Simba Queens ipo kwenye mazungumzo na makocha kutoka nchi tano tofauti akitajwa Birhanu Gizaw, Kocha wa Ethiopia ni kama dili limegeuka na sasa wamemalizana na kumtambulisha Yussif Basigi raia wa Ghana aliyekuwa akiinoa Hasaacas Ladies ya nchini humo.
Awali ilielezwa kuna uwezekano mkubwa wa Gizaw kuja kuwa mrithi wa aliyekuwa kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda lakini sasa Simba ni kama imempotezea na kumgeukia Basigi iliyemtambulisha mchana huu.
Inaelezwa Simba imeshindwana na Muethiopia kwenye mambo ya kimaslahi ambayo alitaka fedha kubwa ilihali timu hiyo haina uwezo wa kumpatia isitoshe wekundu hao wa Msimbazi walihitaji kocha mwenye uzoefu Ligi ya Mabingwa Afrika wakati ambao Gizaw amejizolea umaarufu ukanda wa CECAFA akibeba taji hilo wiki chache zilizopita.
Baada ya kushindwana inaelezwa Simba ikamrudia Mghana waliyepatana kwenye maslahi na ni kocha mwenye CV kubwa CAF.
Kocha huyo wa timu ya taifa ya Ghana inaelezwa ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza baada ya kumaliza mkataba na Hasaacas ambayo tayari ameipa mkono wa kwaheri.
Kocha huyo mwenye Leseni A ya ukocha alijiunga na Hasaacas mwaka 2013 akiweka rekodi ya kocha aliyedumu muda mrefu zaidi kwenye kikosi hicho ambacho amekipa mafanikio mbalimbali.
Ameipatia timu hiyo ubingwa wa Ligi ya Ghana mara nne akichukua miaka mitatu mfululizo msimu wa 2012-13, 2013–14, 2014–15 na 2020–21.
Kimataifa aliisaidia timu hiyo kufuzu Klabu bingwa kwa Wanawake mwaka 2021 ukanda wa WAFU ambapo baadae aliibuka mshindi wa pili baada ya kufungwa na Mamelodi Sundowns kwenye fainali hiyo iliyochezwa nchini Misri kwa jumla ya mabao 2-0.
Kwenye timu za taifa za wasichana mwaka 2015 aliisaidia Black Princess kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake Under-20, Ufaransa 2018, Mashindano ya Michezo ya Afrika 2015, Congo Brazzaville.