Simba ilivyotinga nusu fainali kwa Mkapa

Muktasari:
- Imeshuhudiwa kwa mara ya kwanza Simba inafuzu kwenda hatua ya nusu fainali tangu kuanza kwa mfumo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Dar es Saalam. Hii Tunavuka. Ndiyo kauli ambayo kila shabiki wa Simba aliyekuwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa aliitamka kabla na wakati wa mchezo wa marudiano ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri.
Pengine ungeweza kudhani walikuwa wanapata wapi jeuri ya kutoa ahadi hiyo huku wakijua wana kazi ya kupindua mlima wa mabao mawili waliyoruhusu kule Misri kwenye uwanja wa Suez katika mechi ya mwanzo.

Lakini waliamini katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa ambao mara nyingi umekuwa ukiwakomboa katika michuano ya Kimataifa kwani walijua mechi bado haijaisha.
Muda wa mchezo ulipofika timu zote mbili ziliingia uwanjani kuanza kusakata kandanda ambapo Simba ilianza kwa kasi kulisakama lango la Al Masry huku wachezaji wakipewa nguvu kubwa na mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani.
Kile kilichokuwa kikisubiliwa na mashabiki wengi wa Msimbazi kilianza kuonekana katika dakika ya 22 baada ya Elie Mpanzu kuandika bao la kuongoza.
Dakika 10 baadaye Stephen Mukwala alifunga bao lingine kwa kumalizia mpira wa kichwa uliopigwa krosi na Jean Ahoua bao hilo likidumu hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika.

Kipindi cha pili kilianza huku Al Masry ikionekana kufunguka kulitafuta bao la ugenini ilipofanya majaribio kadhaa kwenye lango la wapinzani wao lakini Simba iliendelea kuutawala mchezo kwa kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hazikuzaa matunda.
Hadi dakika 90 zinamalizika Simba haikufanikiwa kupata bao la tatu licha ya kupata dakika 10 zilizoongezwa kufidia muda uliopotea hasa kutokana na wachezaji wa Al Masry kupoteza muda mara kwa mara.
Baada ya dakika 90 kumaliza yalitengwa matuta ili kumpata mshindi atakayesonga katika hatua ya nusu fainali.

Ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza Simba inafuzu kwenda hatua ya nusu fainali tangu kuanza kwa mfumo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Jean Ahoua, Stephen Mukwala, Kibu Denis na Shomari Kapombe walifunga mikwaju ya penati kwa upande wa Simba.
Katika mikwaju hiyo ya penalti, kipa wa Simba, Moussa Camara aliokoa penalti za Mido Gaber na Mahmoud Hamada huku akifungwa moja na Fakhreddine Ben Youssef