Simba, Coastal Union mechi ya kisasi

Muktasari:
- Lakini la pili ambalo ni kubwa zaidi ni hamu ya kulipa kisasi ambayo kila moja itakuwa nayo kwa mwenzake kutokana na sababu tofauti.
Mambo mawili yanaweza kuifanya mechi baina ya Simba na Coastal Union ya kuwania mshindi wa tatu ikawa na mvuto na ushindani wa aina yake.
Kwanza ni hamu ya kupooza machungu kwa kila upande baada ya kushindwa kutinga fainali ya ngao ya jamii na hivyo kupoteza fursa ya kushinda taji la kwanza msimu huu.
Lakini la pili ambalo ni kubwa zaidi ni hamu ya kulipa kisasi ambayo kila moja itakuwa nayo kwa mwenzake kutokana na sababu tofauti.
Simba ina hasira ya kupokonywa mchezaji Lameck Lawi ambaye ilimsajili kutoka Coastal Union lakini katika hali ya kushangaza, timu hiyo ya Tanga ilibadilisha uamuzi ghafla na kurudisha fedha ilizopewa katika mauzo ya mchezaji huyo na kumuuza Ubelgiji katika timu ya KAA Gent.
Coastal Union yenyewe bila shaka inataka kulipa kisasi cha kupoteza mechi mbili za ligi msimu uliopita dhidi ya Simba ikifungwa mabao 3-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza ugenini na kisha ikapoteza kwa mabao 2-1 nyumbani.
Kocha wa Coastal Union, David Ouma alisema wataivaa Simba kwa namna tofauti na ile waliyocheza na Azam FC.
"Wachezaji wangu wamejifunza katika mechi ile tuliyocheza dhidi ya Azam. Sasa hivi Coastal Union sio timu ndogo tena. Baada ya mechi iliyopita tunatakiwa tugange yajayo ambayo ni mechi dhidi ya Simba na katika mechi hiyo tutakuwa na kikosi cha tofauti kabisa," alisema Ouma.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema wanaingia kwa tahadhari kubwa katika mechi ya leo.
"Tunautazama mchezo huu kama njia mojawapo ya maandalizi ya kutengeneza muunganiko. Kila mechi tunayocheza tunajiandaa kushinda lakini pia hii itakuwa ni fursa nzuri ya kuwatazama na wachezaji wengine," alisema Davids.