Prime
Sababu za Ramovic kufunga virago Yanga
Dar es Salaam. Yanga mambo bado hayajatulia kwenye benchi lake la ufundi na sasa kuna habari zinazokwenda kushtua mashabiki wake. Leo jioni wakati wa mazoezi ya kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, kikijiandaa na mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Jumatano Februari 5, 2025 dhidi ya KenGold utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, kuna habari zikasikika.
Unavyosoma taarifa hii ni kwamba kocha wa Yanga, Sead Ramovic atamalizia mchezo huo wa dhidi ya KenGold kisha atafunga virago vyake na kuondoka Jangwani.
Kuondoka kwa Ramovic kunaelezwa ni baada ya kocha huyo kupata dili kwenye moja ya klabu kubwa iliyopo nchini Algeria.
Waarabu hao si wengine bali ni CR Belouizdad ndio inayomng'oa Ramovic ndani ya Yanga baada ya kumpa dili la maana kwenda kuchukua nafasi ya kocha Abdelkader Amrani aliyeachana na timu hiyo Januari 25, 2025.
Kabla ya Ramovic hajatua CR Belouizdad, kwa sasa inanolewa na Samir Houhou akiwa kaimu kocha mkuu.
Ramovic atakapomaliza kuiongoza Yanga kwenye mchezo dhidi ya KenGold atakuwa amefikisha siku 81 ndani ya klabu hiyo tangu apewe kibarua hicho Novemba 15, 2024 akichukua nafasi ya Muargentina Miguel Gamondi.
Ishu ipo hivi; Kikosi cha Yanga kilikiwa mazoezini leo jioni kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KenGold kesho, Ramovic aliwashtua wachezaji akiwaaga rasmi kwamba baada ya mchezo huo hataendelea kuwa kocha wa timu hiyo hatua ambayo iliwachanganya wengi.
"Ni kweli kocha ametuaga baada ya mazoezi kumalizika, kwakweli imetushtua, kwanza tulidhani labda amegombana na uongozi lakini ameweka wazi kwamba amepata nafasi ya kwenda kufanya kazi sehemu nyingine," amesema mmoja wa mastaa wa timu hiyo.
"Unajua alishaanza kukaa kwenye mioyo yetu, imekuwa ghafla sana kuondoka kwake na unajua bora tungesikia kwanza tetesi lakini amtusapraizi tu baada ya mazoezi na kutuaga."
Katika ujumbe wake Ramovic amewataka wachezaji wa Yanga kupigania pointi tatu za kesho, lakini pia kuhakikisha timu yao inakwenda kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo ameiongoza Yanga kwenye jumla ya michezo 13 ya mashindano yote ikiwemo sita ya Ligi Kuu Bara aliyoshinda yote, sita Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi akishinda miwili, sare mbili na kupoteza mbili, pia mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho (FA) akishinda pia.
Ramovic mpaka anaondoka Yanga alifanikiwa kuongoza msimamo wa ligi kwa saa zisizozidi 24 kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar akiishusha Simba kabla ya wekundu hao kumshusha siku inayofuata ilipoichapa Tabora United kwa mabao 3-0.
Ingawa hakuna kiongozi wa Yanga aliyekubali kueleza taarifa hiyo, lakini tayari Ramovic amewadokeza mabosi wa klabu hiyo juu ya uamuzi wake huo wa kuondoka mara baada ya mchezo wa kesho.
Ramovic kutua kwake CR Belouizdad, atakuwa amemnyima ulaji kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha aliyekuwa kwenye mazungumzo na klabu hiyo kwa takribani wiki moja sasa baada ya kuachana na JS Kabylie.
Wakati Ramovic akiondoka Yanga, nafasi yake inachukuliwa na Abdihamid Moallin ambaye alitambulishwa kikosini hapo Novemba 18, 2024 kama Mkurugenzi wa Ufundi akitokea KMC alipokuwa kocha mkuu.
Hii itakuwa ni timu ya tatu Moallin kuiongoza kama kocha mkuu baada ya kufanya hivyo akiwa Azam kuanzia Julai 2021 hadi Agosti 2022, kisha Julai 2023 hadi Novemba 2024 akiinoa KMC.
REKODI ZA RAMOVIC YANGA
Ligi Kuu Bara: 06
Ushindi: 06
Sare: 00
Kupoteza: 00
Mabao ya kufunga: 22
Mabao ya kufungwa: 02
Kombe la FA: 01
Ushindi: 01
Sare: 00
Kupoteza: 00
Mabao ya kufunga: 05
Mabao ya kufungwa: 00
Ligi ya Mabingwa: 06
Ushindi: 02
Sare: 02
Kupoteza: 02
Mabao ya kufunga: 05
Mabao ya kufungwa: 06
JUMLA:
Mechi: 13
Ushindi: 09
Sare: 02
Kupoteza: 02
Mabao ya kufunga: 32
Mabao ya kufungwa: 08
MATOKEO RAMOVIC AKIWA YANGA
Yanga 0-2 Al Hilal
Namungo 0-2 Yanga
MC Alger 2-0 Yanga
TP Mazembe 1-1 Yanga
Yanga 3-2 Mashujaa
Yanga 4-0 Tanzania Prisons
Dodoma Jiji 0-4 Yanga
Yanga 5-0 Fountain Gate
Yanga 3-1 TP Mazembe
Al Hilal 0-1 Yanga
Yanga 0-0 MC Alger
Yanga 5-0 Copco
Yanga 4-0 Kagera Sugar