Rais Barcelona asema alidhani Messi angeamua kucheza bure

Muktasari:
- Rais wa Barcelona, Joan Laporta ameweka bayana kuwa alitegemea Lionel Messi angebadili mawazo ya kuondoka klabu hiyo na kuamua kucheza bila ya malipo.
Madrid, Hispania (AFP). Rais wa Barcelona, Joan Laporta ameweka bayana kuwa alitegemea Lionel Messi angebadili mawazo ya kuondoka klabu hiyo na kuamua kucheza bila ya malipo.
Messi alijiunga na Paris Saint-Germain Agosti baada ya Barca kuamua kutompa mkataba mpya kutokana na sheria kali za Ligi Kuu ya soka Hispania kuhusu kiwango cha juu cha mishahara.
"Wakati ulikuja ambao pande zote ziliona kuwa isingewezekana. Kila upande ulifadhaika," Laporta alikiambia kituo cha redio cha RAC1.
"Hakutaka kuondoka lakini nao walikuwa katika shinikioz kubwa kwa sababu walipokea maombi mengi. Walijua kama habakii, angekwenda PSG."
"Nilitegemea Messi angebadili uamuzi na angesema nitacheza bure.
"Ningependa hilo na ningelikubali. Navyoona La Liga wangekubali hilo. Lakini hatuwezi kumwambia mchezaji wa kada ya Messi afanye hivyo."
Laporta alisisitiza kuw ahali mbaya kifedha ya klabu ilimaanisha wasingeweza kumbakiza Messi kwa makubaliano yaliyokuwepo awali.
Barca ilipata hasara ya euro 481 milioni (sawa na Sh1.3 trilioni za Kitanzania) msimu uliopita, ikiwa na deni la jumla ya euro 1.35 bilioni.
"Tulikubaliana kufanya ukaguzi (Jumatano) na kwamba kuwekeza kwa Messi kungetuweka hatarini," alisema Laporta, ambaye pia alisema Barcelona bado inaweza kusaini mkataba na kampuni ya uwekezaji ya CVC Capital Partners.
La Liga iliiambia Barca mwezi Agosti kuwa ingeweza kumbakiza Messi kama ikikubaliana na mkataba huo, ambao unahusisha kuuza asilimia 10 ya masuala ya kibiashara, yanayohusisha haki za televisheni, kwa miaka 50 ijayo, kwa euro 2.7 bilioni.
Barcelona, Real Madrid na Athletic Bilbao zilikataa kusaini mkataba huo.
"Hatuhitaji madeni zaidi," alisema Laporta. "Naelewa klabu za La Liga ziko matatizoni. Hatujajiondoa katika operesheni hii, lakini ni lazima wabadilishe. Wanajaribu kuandika upya mkataba."