Pointi tatu za lazima Yanga ikiivaa TP Mazembe leo

Dar es Salaam. Ni ushindi tu ambao kila timu inauhitaji leo wakati Yanga itakapoikaribisha TP Mazembe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
Msimamo wa kundi A la ligi ya mabingwa Afrika ulivyo, unazilazimisha timu hizo kila moja kusaka ushindi leo ili iweke hai matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu huu.
Ikiwa na pointi moja mkiani mwa msimamo wa kundi A, Yanga ina uhitaji mkubwa wa ushindi leo kwa vile ina pointi moja na ikipoteza au kutoka sare leo, itategemea miujiza tu katika mechi mbili zitakazobakia ili iweze kwenda robo fainali kwani itakuwa na uhakika wa kumaliza na pointi saba au nane ambazo timu tatu nyingine kwenye kundi hilo zitakuwa na fursa ya kuzifikia au kuzipita.
TP Mazembe iliyo nafasi ya tatu, ikipata ushindi dhidi ya Yanga leo, ikipata ushindi itafikisha pointi tano ambazo zinaweza kuifanya iipiku au iikaribie MC Alger inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi nne.
Yanga katika mechi ya leo inaingia ikimtegemea Prince Dube ambaye katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti, amehusika na mabao saba, akifunga sita na kupiga pasi moja ya mwisho.
Mchezaji ambaye Yanga inapaswa kumchunga zaidi katika mechi ya leo katika kikosi cha wapinzani wao ni Oscar Kabwit ambaye kati ya mabao sita ya Mazembe katika mechi tano zilizopita, amefunga matatu na kupiga pasi moja ya mwisho.
Urejeo wa kipa Djigui Diarra aliyekuwa majeruhi unategemea kwa kiasi kikubwa kuimarisha safu ya ulinzi ya Yanga kutokana na uzoefu wa mechi za kimataifa ambao kipa huyo raia wa Mali amekuwa nao.
Yanga imekuwa na historia tamu ya kufanya vizuri mechi za kimataifa nyumbani katika miaka ya hivi karibuni na hilo linaweza kujidhihirisha na mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambapo imepata ushindi mara sita na kutoka sare mbili huku ikipoteza michezo miwili.
Wakati Yanga ikiwa tishio nyumbani, TP Mazembe katika mechi 10 zilizopita za kimataifa ugenini walikuwa na unyonge ambapo walipata ushindi mara tatu tu, wakipata sare katika mechi moja na wakipoteza sita.
Yanga inaingia katika mechi ya leo ikiwa inajivunia kiwango na matokeo bora iliyopata katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti ambapo imeshinda nne na sare moja wakati Mazembe yenyewe imekuwa na matokeo ya wastani katika michezo mitano iliyopita ikipata ushindi mara mbili, kutoka sare mbili na kupoteza mechi moja.
Mechi hiyo ya leo itachezeshwa na refa Ahmad Imtehaz Heeralall ambaye atasaidiwa na Ram Babajee na Aswet Teeluck wote kutoka Mauritius huku mwamuzi wa nne akiwa Noris Aaron Arissol kutoka Shelisheli.
Heeralali ni refa mwenye historia ya kumwaga kadi kwa wachezaji watovu wa nidhamu na wale wanaocheza rafu uwanjani.
Katika mechi 18 za mashindano ya klabu Afrika ambayo refa huyo amechezesha, ameonyesha idadi ya kadi 66 ambapo njano ni 64 na kadi nyekundu mbili.
Refa huyo aliwahi kuchezesha mchezo wa mmoja wa Yanga ikiwa nyumbani ilipokutana na Gor Mahia ya Kenya kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na wenyeji kupoteza kwa mabao 2-3 dhidi ya Wakenya hao mechi iliyopigwa Julai 29,2018.
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic alisema kuwa kiwango bora ambacho timu yake imekionyesha katika mechi za hivi karibuni, kinampa imani ya kufanya vizuri leo.
“Tumefunga mabao katika mechi sita zilizopita jambo ambalo ni chanya. Tunacheza dhidi ya timu ngumu.Kujiamini ndio ufunguo lakini kunakuja kutokana na maandalizi, Kama unafanya mazoezi na maandalizi kila siku, kujiamini kunakua na presha inashuka,” alisema Ramovic.
Kocha wa TP Mazembe, Lamine Ndiaye amesema kuwa anafahamu mechi ya leo itakuwa ngumu lakini wana kikosi kizuri cha kuweza kusaka pointi tatu.
“Tunajua kwamba kesho (leo) tutafanya vizuri kwa sababu tumejiandaa. Ni mechi nyingine tofauti na ile iliyopita. Kila mtu ana namna yake ya kujiandaa. Itakuwa mechi nzuri sana ila najua tutapata matokeo,” alisema Ndiaye.