Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pacome shujaa, Yanga ikikamilisha 'hat trick' ya ushindi kwa Coastal Union

Muktasari:

  • Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya pointi 64 katika michezo 24.

Kiungo Pacome Zouzoua amewafanya mashabiki wa Yanga kuondoka na nyuso za furaha katika Uwanja wa KMC Complex, leo Aprili 07, 2025 baada ya kuifungia bao pekee lililoipa ushindi timu yake dhidi ya Coastal Union katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ushindi huo umeifanya Yanga kutimiza mechi ya tatu kupata ushindi dhidi ya Coastal Union msimu huu, ambapo ilipata matokeo kama hayo katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi na kisha ikapata ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya hatua ya 32  bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Kwenye mechi ya leo, Pacome Zouzoua alifunga bao hilo katika dakika ya 35 akimaliza kwa kichwa pasi ya Maxi Nzengeli.

Nzengeli alipokea pasi kutoka kwa Israel Patrick na kupiga pasi hiyo ya juu iliyotua kichwani mwa Pacome na mpira huo kujaa wavuni.

Kabla ya kuruhusu bao hilo Coastal Union iliifanikiwa kuibana vizuri Yanga katika dakika 33 za kwanza ikifunga njia za mipira ya hatari ya wenyeji na kuwaweka kwenye wakati mgumu.

Bao hilo linamfanya Pacome kufikisha mabao nane kwenye ufungaji msimu huu akizidi kusogea juu na kuwakaribia washambuliaji wa timu yake Prince Dube na Clement Mzize wenye mabao 11 kila mmoja.

Wakati timu hizo zinaelekea kumaliza kipindi cha kwanza, Yanga ilipata pigo katika dakika ya 45 baada ya kiungo wake Khalid Aucho kushindwa kuendelea na mchezo akiomba kutoka mwenyewe kufuatia kupata maumivu yaliyoonekana kuwa ya nyama za paja.

Aucho alikuwa anarejea kwenye mchezo wake wa kwanza baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Tabora United kutokana na majeraha aliyopata alipokuwa katika timu ya Taifa lake ambapo jana nafasi yake ilichukuliwa na Mudathir Yahya.

Kipindi cha pili Yanga ilirudi na hesabu za kutaka kutanua ushindi wao ikiganda langoni kwa Coastal Union lakini ikakosa umakini wa kutumia nafasi zake.

Coastal Union ilimrudisha kundini mshambuliaji wake Maabad Maulid ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kusimamishwa na alionyesha mchezo mzuri ambapo alionekana mara kwa mara akiwasumbua mabeki wa Yanga wakiongozwa na nahodha wa Bakari Mwamyeto.

Yanga kwa matokeo hayo imemalizana na Coastal Union msimu huu kwa kuchukua ushindi wa pili lakini mechi zote zikimalizika kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0.