Pacha wa Maxi atajwa kumrithi Aziz Ki

Muktasari:
- Basiala anajua kutoa pasi za mwisho na kuchezesha timu, lakini pia anajua sana kufunga kwa mipira ya adhabu kama ambavyo Aziz KI anafanya.
Dar es Salaam. Misimu miwili iliyopita, mashabiki wa Yanga walidhani ni ndoto kuuzwa kwa mshambuliaji Fiston Mayele lakini Pyramids wakaweka mzigo mezani mwamba akasepa kiroho safi.
Na sasa kituo kinachofuata ni kwa Stepahane Azizi Ki. Presha ya kumuuza kiungo huyo imeanza kukolea ndani ya Yanga na tayari Mwananchi limeambiwa kwamba mezani kwa Yanga wana jina la mbadala wake.
Yanga imevuta waya pale nchini DR Congo kwa Agee Basiala ambaye alikuwa pacha wa Maxi Nzengeli wakati anachezea Maniema ya nchini humo.
Yanga inajipanga kumuuza Aziz KI, mara baada ya msimu huu kumalizika ikitajwa kuwa klabu moja ya nchini Algeria imefika bei ya kutaka kumnunua kiungo huyo na sasa zimeanza hesabu za kutafuta mbadala wake kwani tayari Yanga wameshajua ni kiasi gani watalipwa na wameanza kukipigia bajeti.
Mabosi wa Yanga wamerudi palepale kwanza, Union Maniema ya DR Congo ikionyesha kuvutiwa na huduma ya kiungo wa timu hiyo Agee Basiala ambaye ni staa wa timu hiyo.
Yanga iliwahi kumtaka Basiala msimu mmoja uliopita ikivutiwa na wakati huo akicheza kama kiungo wa pembeni lakini baadaye akabadilishiwa nafasi na kuchezeshwa kama kiungo wa kati mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.
Hapo Maniema ndipo alipotoka Nzengeli na wakati akiwa hapo, alikuwa akichukuliwa kama pacha wa uwanjani na Basiala wote waliifanya Maniema kuwa tishio kabla ya Yanga kuja kumnyakuwa fundi huyo na sasa inataka kummalizia mwingine.
Basiala anajua kutoa pasi za mwisho na kuchezesha timu, lakini pia anajua sana kufunga kwa mipira ya adhabu kama ambavyo Aziz KI anafanya.
Mwananchi linafahamu kuwa, Kiongozi wa Yanga mmoja alipokuwa nchini Morocco kwa majukumu yake kama Mwenyekiti wa Shirikisho la umoja wa klabu ACA, alikutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Maniema Guy Kilongozi wawili hao wakateta juu ya Basiala.
Hatua rahisi kwa Yanga ni kuwa, haihitaji kutumia nguvu sana kumpata mchezaji ndani ya Maniema kwa kuwa tayari ilishatengeneza mahusiano mazuri, kutokana na ukaribu wa viongozi wa timu hizo.
Endapo Yanga itampata Basiala itakuwa imefanya usajili mzuri, kwani kiungo huyo ana nguvu ya kumudu kukimbia eneo kubwa uwanjani kama ilivyo kwa Nzengeli.
Taarifa za ndani zinasema kuwa; “Yanga wanamtaka Agee (Basiala) kweli, tupo nao kwenye mazungumzo bado hayajakamilika, lakini unajua wale ni rafiki zetu wakati wowote kitu kutoka kwao kinaweza kumalizika kwa haraka hakuna shida.
“Unajua sio mara ya kwanza Yanga kumtaka Agee wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu hata wakati rais wao Said (Hersi), alipokuja hapa Congo alimuangalia sana na kuuliza mengi naona sasa hivi wanasema tena wanamtaka,”kilidokeza chanzo chetu ingawa ndani ya Yanga wamekuwa wakifanya siri kubwa kuhusiana na usajili huo.