Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyota timu ya taifa riadha afungiwa miaka 10, sababu yatajwa

Nyota wa timu ya taifa ya riadha, Jackline Sakilu anaripotiwa kufungiwa na Athletics Integrity Unit (AIU) kwa kukutwa na hatia ya kutumia dawa zilizokatazwa michezoni. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa uchunguzi wa AIU, Sakilu alibainika kuwa na viambato vinavyohusiana na homoni ya testosterone, ambavyo ni miongoni mwa dawa zilizopigwa marufuku kwa wanariadha hali iliyokiuka kanuni za kupambana na matumizi ya dawa hizo.

Dar es Salaam. Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limeeleza chanzo cha nyota wa timu ya taifa, Jackline Sakilu kufungiwa na Athletics Integrity Unit (AIU) kwa miaka 10 kujihusisha na riadha.

AIU imetoa adhabu hiyo ikieleza mwanariadha huyo wa mbio ndefu za barabarani (marathoni), amekutwa na hatia ya matumizi ya dawa zilizokatazwa michezoni (doping).

Taarifa ya AIU iliyotolewa mapema wiki hii imeeleza adhabu hiyo imeanza rasmi Septemba 17, 2025 na itadumu hadi mwaka 2035, hatua inayomfanya Sakilu  kukosa mashindano yote ya kimataifa kwa kipindi hicho.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa AIU, Sakilu alibainika kuwa na viambato vinavyohusiana na homoni ya testosterone, ambavyo ni miongoni mwa dawa zilizopigwa marufuku kwa wanariadha hali iliyokiuka kanuni za kupambana na matumizi ya dawa hizo.

Kutokana na ukiukwaji huo, AIU pia imefuta matokeo yote ya Sakilu kuanzia Juni 2024, kabla ya uamuzi huo wa mwisho, Sakilu alikuwa tayari amesimamishwa kwa muda (provisional suspension) mwaka 2025 baada ya vipimo vya awali kuonyesha uwepo wa dawa hizo mwilini mwake.

Mwananchi ilimtafuta mwanariadha huyo bila mafanikio huku Rais wa RT, Rogart Stephen Akhwari akikiri kufungiwa kwa Sakilu.

Amesema RT katika matukio kama hayo huwa inapewa kopi ya adhabu iliyotolewa, akibainisha kwamba kilichomponza Sakilu ni kanuni za AIU na si kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

"Kanuni za AIU zipo wazi kwamba ukitumia dawa za  hospitali ambazo zina element (chembe chembe) ya zile zilizopigwa marufuku michezoni basi utoe taarifa, Jack (Sakilu) wakati huo alikuwa na injury (majeraha) hivyo alikuwa kwenye matibabu," amesema.

Amesema ambacho alikosea ni kutotoa taarifa AIU na katika utetezi wake. mwanariadha huyo alipeleka cheti cha daktari, akibainisha kilichomponza ni kutotoa taarifa na ameadhibiwa kutokana na kanuni," amesema Rogart.

Akitolea mfano baadhi ya dawa, amesema kama zile za asthma, Allergies na hata dawa za maumivu,  mwanamichezo akizitumia na kuzidisha dozi akipimwa utakutwa na hizo element za dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Amesema kesi ya Sakilu ilianza tangu 2024 yeye Rogart akiwa si Rais wa RT.

"Mimi nimechaguliwa 2025, tumelikuta hili jambo na kwa maelezo ya Jack (Sakilu) AIU walikuja kumpima, alijitetea na RT ilimpatia usaidizi lakini ikashindikana," amesema.

Amesema Tanzania ni moja ya nchi bora duniani ambayo haipo kwenye kashfa ya matumizi ya dawa zilizokataliwa na AIU na mwaka huu tumepewa Cheti cha Shirikisho la Dunia (WA).

Katika kesi ya Sakilu, Mwananchi inafahamu katika utetezi wake alisema alitumia dawa za hospitali za nimonia na wakati huo anapimwa hakuwa akikimbia kutokana na kuwa majeruhi.

 Mwanariadha huyo alijitetea mwenyewe kwa maandishi na alihojiwa pia ana kwa ana kabla hukumu haijatolewa na alikubaliana na maamuzi yeyote yatakayotolewa .

Mwananchi inafahamu pia kuwa RT ilimpa msaidizi (translator)wakati wa mahojiano na katika ushahidi wake alipeleka maelezo ya daktari wa hospitali alikotibiwa wakati huo.

Sakilu alikuwa miongoni mwa nyota wa timu ya taifa walioiwakilisha nchi kwenye michezo ya Olimpiki 2024 iliyofanyika, Paris Ufaransa.

Akizungumzia adhabu hiyo, kocha na nyota wa zamani wa timu ya taifa, Suleiman Nyambui amesema ni fedhea kwa taifa akishauri kitengo cha kupambana na dawa zilizozuiwa michezoni ambacho kipo chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kulifuatia kwa kina suala la dawa hizo kwa wananimichezo wa Tanzania.

"Hii si mara ya kwanza kutokea, huko nyuma wapo waliowahi kufungiwa, sema kwa Sakilu imekuwa adhabu kubwa zaidi," amesema Nyambui.

Amesema vitendo hivyo kwa wanamichezo vinafanyika aidha kwa kujua au kutokujua, hivyo ilipaswa BMT kupitia kitengo cha kudhibiti dawa hizo ikalisimamia na kutoa elimu kwa wanamichezo.