Neymar ampiga kofi mtoto wa Robinho mazoezini
Mshambuliaji wa Santos FC, Neymar Jr (Kulia), mwingine pembeni ni Kinda wa timu hiyo, Robinho Jr. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Tukio hilo limetokea wakati wachezaji wote wawili walikuwa sehemu ya kikosi cha akiba, baada ya kutochezeshwa katika mchezo wa ligi dhidi ya Palmeiras.
Mshambuliaji wa Santos FC, Neymar Jr anaripotiwa kuzua mzozo katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo baada ya kumshambulia mchezaji mwenzake kinda, Robinho Jr.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka vyombo vya habari vya Brazil, tukio hilo limetokea baada ya Neymar kukerwa na kitendo cha kupigwa chenga na kinda huyo mwenye umri wa miaka 18, ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Brazil, Robinho.
Inaelezwa kuwa baada ya tukio hilo, Neymar alimwambia Robinho Jr apunguze kasi ya mchezo, hali iliyosababisha mabishano kabla ya wawili hao kusukumana.
Ripoti zinaeleza kuwa mzozo huo uliendelea hadi Neymar alipompiga kofi na kumwangusha chini mchezaji huyo, kabla ya wote wawili kutolewa kwenye mazoezi.
Baadaye, wawakilishi wa Robinho Jr walifikisha malalamiko yao kwa uongozi wa klabu, lakini suala hilo limemalizika baada ya Neymar kuomba radhi na kukiri makosa yake.
Inaelezwa pia kuwa wawili hao wana uhusiano wa karibu nje ya uwanja, unaofanana na ule wa Baba na Mtoto wa kiroho.
Tukio hilo limetokea wakati wachezaji wote wawili walikuwa sehemu ya kikosi cha akiba, baada ya kutochezeshwa katika mchezo wa ligi dhidi ya Palmeiras.
Kwa upande mwingine, Neymar anaendelea kupambana kurejea kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil, huku akihitaji kuthibitisha ubora wake kabla ya michuano mikubwa ya Kombe la Dunia kuanza huko Marekani, Canada na Mexico.
Mchezaji huyo amekuwa akikabiliwa na changamoto za majeraha katika miaka ya karibuni, huku akitafuta kurejesha kiwango chake akiwa Santos.
Wakati huohuo, Robinho Jr anaendelea kujijenga ndani ya kikosi cha kwanza cha Santos, akitafuta kufuata nyayo za Baba yake licha ya changamoto zinazoikabili familia yake.