Mpishi amburuta Neymar mahakamani akimdai Sh129 milioni
Nyota wa Brazil, Neymar.
Muktasari:
- Neymar amezichezea klabu nne tu katika maisha yake ya soka la kulipwa ambazo ni Santos, Barcelona, PSG na Al Hilal.
Nyota wa Brazil, Neymar amefikishwa katika vyombo vya kisheria na aliyewahi kuwa mpishi wake akidaiwa kiasi cha Pauni 37,544 (Sh129 milioni) kwa kosa la kumfanyisha kazi nje ya muda wa makubaliano ya mkataba wakati alipokuwa akimhudumia.
Mpishi huyo anadai kwamba Neymar alikuwa akimzidishia kazi na muda wa kumpikia tofauti na ule waliokubaliana jambo ambalo limemuathiri kimwili na kiakili.
Neymar ametuhumiwa kumfanyisha kazi kwa saa 16 mpishi huyo huku pia akimlazimisha kupika chakula cha kulisha marafiki zake wapatao 150 kwa siku tofauti na makubaliano.
Hata hivyo kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mpishi huyo alitakiwa kufanya kazi kwa saa 10 kwa siku kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi na siku ya Ijumaa alitakiwa kufanya kwa saa tisa.
Hata hiyo mpishi huyo anadai kwamba Neymar alimlazimisha kufanya kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 5:00 usiku na pia hadi siku za mwisho wa wiki.
Mpishi huyo amedai kwamba kuna wakati alikuwa analazimishwa kufanya kazi hadi katika muda wake wa kisheria wa kupata chakula cha mchana.
Kutokana na uzito wa majukumu aliyokuwa anapewa. mpishi huyo amedai kwamba kwa sasa amepata matatizo ya maumivu ya mgongo na nyonga.
Na sasa mpishi huyo ambaye alikuwa analipwa kiasi cha Pauni 1,065 (Sh3.7 milioni) kwa mwezi anataka alipwe fidia kwa athari alizopata.
Neymar ambaye kwa sasa anaichezea Santos, amekutana na mashataka hayo katika kipindi ambacho anajaribu kupigania fursa ya kuwepo katika kikosi cha Brazil kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia baadaye mwaka huu huko Marekani, Canada na Mexico.