Kisa kipigo, Neymar aangua kilio hadharani
Muktasari:
- Hiki ni kichapo kikubwa zaidi, Neymar anakutana nacho katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.
Santos, Brazil. Nyota wa Brazil, Neymar Jr juzi alitoka uwanjani akiwa anabubujikwa na machozi baada ya timu yake, Santos, kupokea kipigo cha aibu cha mabao 6-0 kutoka kwa Vasco da Gama.
Hiki ni kichapo kikubwa zaidi, Neymar anakutana nacho katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.
Neymar, mwenye umri wa miaka 33, alirejea katika klabu yake ya utotoni, Santos, mapema mwaka huu baada ya kipindi kigumu cha miezi 18 katika klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia kilichojaa majeraha na changamoto nyingi.
Ingawa amekuwa na mchango wa wastani tangu arejee Brazil, akifunga mabao sita na kutoa pasi tatu za mabao katika mechi 19 hali ya klabu yake si nzuri.
Santos wanashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ya Brazil, wakiwa alama mbili tu juu ya mstari wa kushuka daraja.
Lakini hali hiyo ilizidi kuwa mbaya Jumapili, wakati walipofungwa mabao 6-0 na Vasco da Gama, huku mchezaji wa zamani wa Liverpool, Philippe Coutinho, akifunga mabao mawili.
Kipigo hicho kiliwaacha mashabiki na wachezaji wa Santos katika mshtuko na Neymar, akiwa mmoja wao, aliangua kilio hadharani uwanjani baada ya filimbi ya mwisho.
Akiwa amejawa na huzuni, Neymar alionekana akifuta machozi kwa jezi yake kabla ya kuondoka uwanjani akiwa amefuatana na mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi ambaye alijaribu kumfariji.
Akizungumza baada ya mechi hiyo ya aibu, Neymar hakuweza kuficha hasira na masikitiko yake:
"Ninaona aibu," alisema kwa uchungu.
"Nimekatishwa tamaa kabisa na uchezaji wetu. Mashabiki wana kila haki ya kuandamana na kulalamika, ilimradi tu wasitumie vurugu lakini kama wanataka kutukana na kulaani, wako sahihi."
Aliendelea kwa kusema:
"Ni hisia za aibu ya hali ya juu. Sijawahi kupitia kitu kama hiki maishani mwangu. Kwa bahati mbaya, kimetokea. Machozi yalikuwa ya hasira na kila kitu. Siwezi kusaidia kila mara. Kwa kweli, hali ilikuwa ya hovyo kabisa, hiyo ndiyo hali halisi."
Hapo awali, kipigo kikubwa zaidi katika maisha ya Neymar kilikuwa mwaka 2015, alipokuwa Barcelona, walipofungwa 4-1 dhidi ya Celta Vigo katika La Liga.
Mara tu baada ya kichapo hicho dhidi ya Vasco, uongozi wa Santos ulitangaza kumfuta kazi kocha mkuu Cleber Xavier, katika juhudi za kuokoa msimu wao.
Neymar, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Brazil, alisaini mkataba na Santos mwezi Januari 2025, akiwa na nia ya kurudi katika kiwango chake bora kuelekea Kombe la Dunia la 2026.
Mwezi Juni, aliongeza mkataba wake hadi mwishoni mwa mwaka huu, huku kukiwa na chaguo la kuongeza miezi mingine sita.
Rais wa klabu, Marcelo Teixeira, alieleza kuwa kurejea kwa Neymar kumeleta mafanikio makubwa ya kibiashara kwa Santos pamoja na ongezeko kubwa la wafuasi katika mitandao ya kijamii.
“Shujaa wetu, kijana wetu, mtoto wa nyumbani, mwenye jezi namba 10 atasalia nasi,” alisema.
Baada ya kipigo hicho kizito, Santos sasa nwanakabiliwa na mtihani mwingine mkubwa watakapomenyana na Bahia Jumapili ijayo.