Napoli yatwaa ubingwa Seria A, Inter kujiuliza UCL

Muktasari:
- Conte ameweka rekodi ya kutwaa taji hili akiwa na Klabu tatu tofauti kwenye Ligi hiyo ambazo ni Juventus, Inter Milan na sasa Napol.
Italia. Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cagliari umetosha kuipa Napoli ubingwa wa Ligi Kuu Italia ‘Seria A’ msimu wa 2024/25.
Napoli imenyakua taji hilo ikiwa na pointi 81 baada ya mechi 38 ikiwa ni tofauti ya pointi moja na Inter Milan ambayo imemaliza nafasi ya pili na pointi 80.
Mabao ya Napoli yamefungwa na Scott McTominay na Romelu Lukaku ambayo yameipa ubingwa wa nne kwa ‘Gli Azzuri’ inayonolewa na kocha Antonio Conte.
Conte ameipa Napoli taji hilo ikiwa ni msimu wake wa kwanza baada ya kujiunga na miamba hiyo Juni 2024 kwa kandarasi ya miaka mitatu.
Kocha huyo aliichukua Napoli ikiwa na hali mbaya baada ya msimu wa 2023/24 kumaliza ktika nafasi ya 10 baada ya kushindwa kutetea ubingwa wao wa 2022/23 chini ya kocha Luciano Spalletti.
Ubingwa huu unaifanya Napoli kufikisha mataji manne ya Serie A kwani mara ya mwisho ilichukua ubingwa msimu wa 1986-1987, 1989-1990, 2022-2023, na sasa 2024 - 2025.
Conte ameweka rekodi ya kutwaa taji hili akiwa na Klabu tatu tofauti kwenye Ligi hiyo ambazo ni Juventus, Inter Milan na sasa Napol.
Kiungo wa Napol, Scott McTominay amefanikiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya Seria A (MVP). Mchezaji huyo raia wa Scotland ameweka rekodi ya kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza Italia tangu ajiunge nayo akitokea Manchester United.
McTominay ameisaidia Napol katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu kwani amehusika katika mabao 15 akifunga 11 na kutoa pasi nne za mabao.
Kwa upande wa mfungaji bora, tuzo hiyo imekwenda kwa mshambuliaji wa Atalanta, Mateo Retegui ambaye amefunga mabao 25 katika mechi 35 alizocheza msimu huu.
Retegui ameonyesha kiwango bora msimu huu akiwashinda Moise Kean wa Fiorentina mwenye mabao 18, Ademola Lookman (Atalanta, mabao 15), Marcus Thuram (Inter Milan, mabao 14) pamoja na Riccardo Orsolini (Bologna, mabao 14).
Mfungaji bora msimu uliopita alikuwa ni Lautalo Martinez wa Inter Milan ambaye safari hii ameishia katika nafasi ya saba akiwa amefunga jumla ya mabao 12.
Inter imebakisha Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo itacheza fainali dhi ya PSG Mei 31, mwaka huu kama tegemeo lao pekee kwa msimu wa 2024/25 baada ya kutoka weupe bila kombe nyumbani.
Timu iliyoshuka daraja mpaka sasa ni Monza ambayo inabuluza mkia ikiwa imekusanya jumla ya pointi 18 katika michezo 37 huku Venezia, Empol, Lecce na Parma zikisubili mechi za mwisho kujua hatima yao ni ni timu gani itashuka au kubaki kwenye Ligi hiyo.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa michezo miwili kati ya Bologna ambayo itakuwa nyumbani dhidi ya Genoa pamoja na AC Milan dhidi ya Monza wakati kesho Jumapili, Mei 25 timu zote zilizosalia zitashuka dimbani kucheza michezo ya mwisho ya kumaliza ratiba ya msimu huu wa 2024-2025.