Prime
MZEE WA FACT: Mpira zaidi ya uujuavyo

Ukiangalia nembo ya Shirikisho la Soka hapa nchini, TFF, utaona imemeandikwa ‘Tanzania Football Federation’ halafu ikatafsiriwa kwa Kiswahili na kuandikwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.
Hili ni kosa kubwa. Football siyo mpira wa MIGUU, ni mpira wa MGUU...foot siyo feet!
Watu wengi (wakiwemo TFF), hudhani mchezo huu unaitwa Football kwa sababu wachezaji hutumia miguu uwanjani, la hasha!
Hakuna uhusiano wowote kati ya kucheza kwa kutumia miguu na jina la mchezo huu.
Narudia, hakuna uhusiano wowote kati ya jina la mchezo huu na uchezaji wa kutumia miguu!
Sheria za soka zilitungwa 1863 huko England ambapo pia kuliundwa chama cha soka ili kuzisimamia.
Moja ya sheria hizo ilikuwa kukataza matumizi ya mikono, hii ina maana kwamba hapo kabla, mikono ilitumika na bado mchezo huu uliitwa Football.
Katika ubinadamu wetu wa kawaida, endapo mtu hatabanwa na sheria katika kutumia kiungo chochote, hakuna kiungo atakachokitumia zaidi kuliko mikono.
ASILI
Kabla ya kutungwa kwa sheria moja itakayosimamia mchezo huu dunia nzima, watu walicheza kiholela, kila timu ilikuwa na sheria zake.
Ilipotokea timu mbili zinacheza, kila moja ilicheza kwa mujibu wa sheria zake ikawa vurugu ikawa shida.
Moja ya shida hizo ilikuwa kipimo cha mpira utakaotumika. Kila timu ilikuwa na kipimo cha mpira wake.
Kwa hiyo kabla mechi haijaanza, kulikuwa na mabishano makubwa juu ya mpira gani utumike.
Kila timu ilitaka utumike mpira wao, wakati mwingine mechi hazikufanyika na kuzua ugomvi mkubwa.
Utata huu ukamlazimu mfalme wa Uingereza kutoa agizo la kutengenezwa kipimo kimoja cha mpira kitakachotumika na wote.
Mfalme huyo akajitolea sehemu ya chini ya mguu wake (foot), ipimwe ili itumike kama kipenyo cha mpira utakaotengenezwa.
Mpira ulipotengenezwa ukawa na kipimo cha kipenyo cha mguu, hivyo ukaitwa Football. Hapo ndipo jina la mchezo huu lilipoanzia.
Kwa hiyo Football imetokana na mguu (foot), wa mfalme, siyo miguu (feet).
Kusema Mpira wa Miguu ni kosa ni Mpira wa Mguu! Ni Football, siyo Feetball.
FIFA
FIFA ni kifupisho cha maneno ya lugha ya Kifaransa ambayo ni Fédération Internationale de Football Association.
Tafsiri ya Kiingereza cha moja kwa moja ya maneno haya ni International Federation of Association Football.
Kwa hiyo, kama tungeita kwa Kiingereza, FIFA, ingekuwa IFAF.
Kwa tafsiri ya Kiswahili, FIFA au IFAF, ni Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Mguu.
Watu wengi hudhani FIFA ni Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Mguu, la hasha, vyama havijatajwa hapo.
Hiyo Association Football iliyopo kwenye FIFA(IFAF), ndiyo mpira wenyewe!
UFAFANUZI
Jina kamili la mpira wa mguu kwa Kiingereza ni Association Football, siyo tu Football.
Hii inatokana na asili ya mchezo huu.
Hapo zamani za kale, mchezo huu haukuwa na sheria wala chama cha kuusimamia mpaka mwaka 1863 zilipotungwa sheria na kuundwa chama cha kwanza cha mpira wa miguu, FA, huko England.
Moja ya sheria zilizotungwa ilikuwa kukataza matumizi ya mikono, kuushika mpira au kumshika mchezaji wa timu pinzani.
Baadhi ya wachezaji ambao walishazoea kucheza bila sheria, ambapo matumizi ya mikono yalikuwa ruksa, wakapinga sheria hizi.
Watu hao wakakataa kuwa chini ya FA na kuanzisha chama chao walichokiita Football Union (FU), ambacho kiliruhusu matumizi ya mikono.
Kwa hiyo kukawa na Football mbili, ile inayosimamiwa na FA ambayo matumizi ya mikono yalikatazwa, na ile inayosimamiwa na FU ambayo matumizi ya mikono yaliruhusiwa.
Ile Football ya FA ikaitwa Association Football yaani Football ya Association na ndiyo hii iliyopo chini ya FIFA mpaka sasa.
Ile Football nyingine ya FU ikaitwa Union Football yaani Football ya Union.
Baadhi ya wachezaji wa Football ya Union, wakahamia Marekani na kuipeleka huko ambako siku hizi inaitwa American Football.
Wale waliobaki England wakaibadili jina na kuiita Rugby. Kisa cha kuiita hivyo ni kitendo cha mchezo huo kutawaliwa na shule moja iliyoitwa Rugby kiasi cha watu kuona kama mchezo huu ulikuwa maalumu kwa ajili ya shule hiyo.
USHAHIDI
Kwenye Ligi ya England, kuna timu inaitwa AFC Bournemouth. Kirefu cha AFC ni Association Football Club.
Mji inakotoka timu hii wa Bournemouth, kuna timu mbili za Football; moja ya Football ya Association (ndiyo hiyo AFC Bournemouth), na nyingine ya Football ya Union inayoitwa Bournemouth Rugby Football Club.
Klabu ya Aston Villa, ilikumbwa na tetemeko kubwa la mgawanyiko huu.
Wakati watu wa FU wanajitenga na FA, klabu hii ikagawanyika sehemu mbili, wapo wanachama waliotaka klabu yao ijiunge na FA na wengine walitaka ijiunge na FU.
Ikabidi wakubaliane kucheza mechi mbili maalumu, moja ya Association Football na nyingine ya Union(Rugby) football.
Wanachama watakaokuwa washindi wa jumla, mchezo wao ndiyo utakaotambulika klabuni. Walipocheza, watu wa Association Football wakashinda na klabu hiyo mpaka sasa inacheza Association Football.
Nchini Italia kuna klabu inaitwa AC Milan. Kirefu chake ni Associazione Calcio Milan. Calcio ni Football kwa Kiitaliano, kwa hiyo AC Milan, kwa Kiingereza, ni Association Football Milan.
SOKA
Kusema Association Football au Union Football, ikaanza kuwa kero kwa watu kwa sababu ya urefu wa maneno hayo.
Watu wakaanza kuyakatisha, wakawa hawalitaji neno Football kwa sababu linajirudia kote kote, kwenye Association na kwenye Union. Kwa hiyo badala ya kusema Association Football, wakasema tu Association. Na badala ya kusema Union Football, wakasema tu Union.
Mwishoni mwa karne ya 19, kulizuka aina fulani ya mtindo wa kukatisha maneno nchini England, ulioanzia Chuo Kikuu cha Oxford.
Ukatishaji huu wa maneno unafanana na ule uliozuka hapa nchini Tanzania mwanzoni mwa karne ya 21 ambapo vijana waliongeza neno ‘nga’ katikati ya jina refu ili kulifupisha. Hapa ndipo shule zilipoitwa Skonga, yaani kifupisho cha school (scho) na kuongeza ‘nga’ mbele.
Kikwete akaitwa Kikwenga...Sepetu akaitwa Sepenga, nk.
Na England pia kulikuwa na namna yake ya kukatisha maneno. Wao waliongeza herufi ‘er’ katikati ya kifupisho cha jina refu. Lakini herufi ya mwisho kwenye kifupisho, waliirudia mara mbili. Yaani kama kifupisho kiliishia na herufi ‘p’ basi watairudia hiyo ‘p’ mara mbili na kuwa ‘pp’ halafu wanaongeza ‘er’ mbele na kuwa ‘...pper’
Kwa hiyo, jina refu la Association, wakalikatisha na kuishia Assoc...ile herufi ya mwisho kwenye kifupisho ni ‘C’, wakairudia mara mbili na kuongeza ‘er’ mbele kwa hiyo ikawa Assoccer. Hapo ndipo lilipoanzia neno Soka.
RAGA
Mtindo huu haukuwaacha salama wale wa Union. Kwa kuwa mchezo wao tayari ulishabadilika na kuitwa Rugby kama tulivyoona kule juu, basi wakalikatisha hilo neno Rugby na kuwa Rugger. Kanuni ni ile ile, unairudia mara mbili herufi ya mwisho kwenye kifupisho halafu unaongeza ‘er’ mbele. Kwa hiyo neno Rugby walilikatishia kwenye ‘g’ na kuwa rug...wakairudia ‘g’ mara mbili ikawa rugg...wakaongeza ile ‘er’ na kupata rugger. Hili ni jina linalotumika mpaka sasa kuutambulisha mchezo huu.
REFARII (REFEREE)
Kitabu cha sheria za soka (Laws of the game) kiliandikwa 1863 baada ya kuanzishwa kwa chama cha soka England, FA. Kabla ya hapo, hakukuwa na sheria za mchezo huu.
Baada ya kuanzishwa sheria, likaja tatizo ya kuzitafsiri uwanjani. Sheria hizo zilikuwa mpya na ngeni hivyo hakukuwa na mtu aliyezijua zote kwa mara moja. Ilibidi utumike utaratibu wa kuwa na mtu wa kusaidia kuzitafsiri kwa msaada wa kitabu, huku mechi ikiendelea.
Wakati wa mchezo, kukawa na mtu anayekaa nje na kitabu cha sheria na panapotokea uvunjifu wa sheria za mchezo, mechi ilisimama, wachezaji walienda nje kwa mtu mwenye kitabu cha sheria na kufanya mrejeo wa sheria kwa mujibu wa kitabu.
Kwa Kiingereza, kufanya mrejeo au kurejea ni ‘refer’ na mtu ambaye hutumika kwa ajili ya kurejea au kufanya mrejeo huitwa referee. Hapo ndipo lilipoanzia jina la waamuzi kuitwa marefarii.
Kitendo cha mechi kusimama halafu wachezaji wanaenda nje kwa ajili ya kurejea sheria, kuliwakwaza wachezaji na mashabiki kwamba kulipoozesha mchezo na kupunguza ladha.
Ikaamuliwa yule mtu wa kufanyia mrejeo, yaani ‘referee’, ajifunze sheria zote na aziweke kichwani ili aingie uwanjani na kuzitafsiri wakati mchezo ukiendelea badala ya kukaa nje na kitabu.
Kuanzia hapo, wale watu wa kurejea sheria, wakawa wanaingia uwanjani.