Mukwala, Aucho waitwa Uganda Afcon

Muktasari:
- Kocha wa Uganda Paul Put ameita kikosi hicho chenye mchanganyiko wa wachezaji wanaocheza katika klabu za Uganda na wale wa timu za nje ya nchi hiyo.
Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho na mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala wameitwa katika kikosi cha Uganda kinachojiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Kocha wa Uganda Paul Put ameita kikosi hicho chenye mchanganyiko wa wachezaji wanaocheza katika klabu za Uganda na wale wa timu za nje ya nchi hiyo.
Katika kundi hilo amewajumuisha Aucho na Mukwala ambao walikuwemo kikosini pindi timu hiyo ilipocheza mechi mbili zilizopita za kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Botswana na Algeria.
Timu hiyo itacheza na Afrika Kusini, Septemba 6 ikiwa ugenini na baada ya hapo, Jumatatu Septemba 9, Uganda itakuwa nyumbani kuikabili Congo kwenye Uwanja wa Namboole na baada ya hapo kambi itavunjwa na wachezaji kurejea kwenye klabu zao.
Idadi kubwa ya wachezaji walioitwa ni mabeki ambapo wameitwa 11, washambuliaji wakiwa wanane, viungo sita na makipa watatu.
Kikosi cha Uganda kinaundwa na makipa Isima Watenga, Alionzi Nafiani na Charles Lukwago.
Mabeki ni Elvis Bwomomo, James Begisa, Isaac Muleme, Joseph Ochaya, Abdul Azizi Kayondo, Bevis Mugabi, Elio Capradossi, Halidi Lwaliww, Ardord Odongo, Timothy Awanya na Kenneth Semakula.
Viungo walioitwa ni Aucho, Bobosi Byaruhanga, Joel Sserunjogi, Ronald Sakiganda, Travis Mutyaba na Saidi Mayanja.
Nyota wanaounda safu ya ushambuliaji ni Dennis Omedi,Jude Ssemugabi, Joackim Ojera, Rogers Mato, Muhammad Shaban, Mukwala, Calvin Kabuye na Allan Okello.
Wakati huohuo kipa wa Simba, Moussa Camara ni miongoni mwa wachezaji 23 walioteuliwa na kocha wa Guinea, Charles Paquile kwa ajili ya kujiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) mwezi ujao dhidi ya DR Congo na Tanzania ‘Taifa Stars’ mwezi ujao.
Guinea maarufu kama Syli National itaanza ugenini kwa kuivaa DR Congo, Septemba 6 na baada ya hapo itakuwa nyumbani kuikabili Taifa Stars, Septemba 10.
Kiwango bora ambacho Camara ameanza nacho katika kikosi cha Simba iliyomsajili mwezi huu akitokea Horoya, kimelishawishi benchi la ufundi la Guinea kuendelea kumjuisha kikosini kama lilivyofanya katika mechi mbili zilizopita za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Algeria na Msumbiji.
Mwingine aliyeitwa kutoka Simba ni Mbukinafaso Valentin Nouma ambapo nchi yake itavaana na Senegal Septemba 6 na Septemba 10 dhidi ya Malawi.