Mbrazil aivurugia Simba ramani

Dar es Salaam. Baada ya kuumia kwa kipa mpya, Jefferson Luis, Simba imeanza kutafuta mwingine, ambaye imepanga kumshusha kutoka moja ya nchi tatu zilizopo Bara la Amerika, huku mchakato huo ukiwavuruga viongozi.
Simba ilimsajili Jefferson kama mrithi wa Beno Kakolanya aliyetimkia Singida Fountain Gate, akifanya kazi ya Aishi Manula anayeuguza majeraha ya nyonga yatakayomuweka nje hadi Novemba, lakini baada ya mazoezi ya siku mbili, Jefferson alipata majeraha yatakayomuweka nje kwa muda mrefu.
Wekundu wa Msimbazi wamechungulia sokoni kwa makipa wa Afrika na kugundua ni ngumu kumpata kwa haraka, wakakumbuka kuna majina ya makipa wakali waliwahi kupewa na mawakala kutoka nchi tatu za El Selvador, Venezuela na Peru, zote zikiwa za Amerika.
Ni rasmi Simba imeanza kufanya mchujo wa makipa hao ikitafuta mmoja, ambaye ataungana na Ally Salim na Ahmed Feruz aliyepandishwa kutoka timu ya vijana.
Hata hivyo, Simba italazimika kumlipa Jefferson ili kuvunja mkataba wake alioingia wiki mbili zilizopita, lakini pia itamlipa stahiki nyingine ambazo anastahili kutokana na mkataba wake ulivyo.
Hilo si jambo gumu kwa Simba na tayari imeanza mazungumzo na Jefferson ili kumalizana kwa amani na leo anatarajiwa kurejea Brazil.
Awali, Simba ilikuwa na mpango wa kuwarudia makipa watatu iliokuwa imeanzisha mazungumzo nao kabla ya kumsajili Jefferson, lakini imewapiga chini na sasa akili yao inachakata majina ya makipa wapya kutoka El Selvador, Venezuela na Peru.
Makipa ambao awali Simba ilitaka kuwarudia ili wachukue mikoba ya Jefferson ni Caique Da Santos, ambaye alishindwa kutua Simba kutokana na kuhitaji pesa nyingi, lakini pia lugha ikitajwa kuwa changamoto.
Mwingine ni Simon Omossola wa Cameroon, aliyewahi kuichezea AS Vita, lakini kwa sasa anakipiga Saint Eloi Lupopo ya DR Congo na Coast Issa Fofana wa Ivory Coast kutoka Al Hilal ya Sudan, ambayo Simba imetajiwa pesa nyingi ili kumnunua jumla.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alithibitisha timu yake kuingia sokoni kutafuta kipa kama ambavyo imesema ripoti ya daktari ya jana.
"Leo (jana), ndipo tutapata ripoti ya mwisho ya daktari. Kama jeraha lake litakuwa la muda mrefu basi hatutasubiri, lazima tutaingia sokoni kutafuta kipa mpya haraka iwezekanavyo," alisema Ahmed.
Simba itakutana na changamoto nyingine ya kupata kipa wa kiwango cha juu katika wakati huu ambao timu nyingi zilishaanza kujiimarisha, huku pia ikilazimika kumlipa Jefferson, aliyeumia.
Lakini suala jingine ni kwa Simba ni jinsi ya kukimbizana na muda uliopo wa usajili wa CAF.