Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matokeo ya Man United Pre Season yashtua

Wachezaji wa Liverpool, Mohamed Salah na Cutis Jones wakishangilia bao dhidi ya Manchester United katika mechi iliyomalizika kwa Liverpool kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Muktasari:

  • . Manchester United, baada ya kuweka kambi ya maandalizi nchini Marekani na kucheza michezo ya kirafiki, inakabiliwa na hofu kutokana na matokeo mabaya mechi hizo.

Manchester, England. Manchester United iliweka kambi ya maandalizi ya msimu nchini Marekani na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki.

Baada ya kushindwa kufanya vizuri msimu uliopita, mashabiki wa timu hiyo wamekuwa na imani kuwa kikosi chao kinaweza kufanya vizuri msimu ujao kutokana na mabadiliko yaliyopo.

Hata hivyo, timu hiyo itaanza kuonyesha picha halisi kwenye mchezo wa wikiendi ijayo itakapovaana na Manchester City kwenye mchezo wa ngao ya Jamii utakaopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.

Pamoja na timu hiyo kumaliza msimu kwa kishindo kwa kutwaa Kombe la FA na kupata nafasi ya kucheza michuano ya Europa msimu huu, bado mashabiki wameanza kupata hofu na kikosi hicho kutokana na kufanya vibaya kwenye michezo ya maandalizi ya msimu mpya.

Michezo ya Manchester United ya kujiandaa na msimu haikuwa na matokeo mazuri, ingawa siyo kipimo sahihi kuwa timu hiyo itafanya vibaya kwenye ligi msimu ujao.

United ilianza kwa kupata kichapo nchini Norway baada ya kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Rosenborg ambapo baada ya mchezo huo kocha Erik ten Hag alisema kuwa hawajaonyesha kiwango cha timu kubwa kama ilivyo United.

Wachezaji wa Manchester United wakishangilia moja ya bao kati ya matatu yaliyowapa ushindi dhidi ya Real Betis Agosti Mosi, 2024.

Baada ya mchezo huo, United ambayo ni timu yenye rekodi kubwa kwenye Ligi Kuu England ililala tena kwa mabao 3-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Liverpool kwenye mchezo uliopigwa nchini Marekani.

Baada ya mechi hiyo United iliibuka na ushindi dhidi ya Rangers na Real Betis na baadaye ikalala kwa mabao 2-1 dhidi ya Arsenal kwenye mchezo wenye malalamiko mengi.

Mashabiki wa Man United wanawalaumu wachezaji wa Arsenal kuwa walikwenda kwenye mchezo huu kwa nia moja tu ya kuwaumiza wachezaji wao baada ya dakika tisini kumaliza kwa mastaa wa United, Rasmus Hojlund na Leny Yoro kupata majeraha.

Pamoja na kwamba Rasmus anaonekana kuwa anaweza kurejea uwanjani vizuri, lakini beki mpya wa timu hiyo Yoro taarifa zinasema kuwa jeraha hilo litamweka nje ya uwanja kwa miezi mitatu na zaidi.

Hata hivyo, kocha wa timu hiyo amekuwa akijitetea kutokana na matokeo aliyopata baada ya kusema kuwa wachezaji wake wengi hawakuwepo kwenye maandalizi ya msimu baada ya kuwa kwenye michuano ya Euro na Copa Amerika hivyo kilichoonekana kwenye maandalizi ya msimu siyo uhalisia wa kikosi chao.

United sasa itaingia kwenye mchezo wa Ngao Jumamosi na bado inaonekana kuwa itawakosa baadhi ya mastaa wake kama ilivyo kwa Man City.

Hata hivyo, kumbuka kuwa United ilifanikiwa kuichapa City kwenye mchezo wa mwisho waliokutana kwenye fainali ya Kombe la FA msimu uliopita lakini maandalizi yao ya msimu yameonekana kudhorota.

Katika mchezo wa mwisho wa maandalizi ya msimu mpya City yenyewe ilionyesha kiwango cha juu baada ya kuichapa Chelsea mabao 4-2, ikionekana kuwa inaweza kufanya mambo makubwa kwenye ngao na mechi za ligi.

Mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Jesus akimtoka beki wa Manchester United Leny Yoro wakati ya mechi ya kirafiki iliyochezwa nchini Marekani.

Pre Season mbaya kwa miaka sita:

Kwa upande wa matokeo hiki ndiyo kipindi ambacho United imefanya vibaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule kwa kipindi cha miaka sita tangu msimu wa 2018-19, wakati kocha Jose Mourinho alipokuwa bosi kwenye benchi la ufundi la timu hiyo.

Kipindi hiki United ilifanikiwa kushinda mchezo mmoja tu kati ya sita ya maandalizi ya msimu kikiwa kipindi kibaya zaidi ambacho kiliwafanya mashabiki kupunguza kasi ya kuifuatilia timu hiyo na kuamini kuwa itafanya vibaya kwenye ligi.

Hata hivyo, pamoja na mambo yote inaonekana kuwa majeraha ya Yoro na Hojlund yanaweza kuwa sababu ya United kushindwa kufanya vizuri kwenye michezo yake, hata hivyo mashabiki wamekuwa na maoni toifauti wakitaka timu hiyo iingie sokoni kuboresha kikosi chake.