Mastaa Ligi Kuu wapigwa chini Taifa Stars

Muktasari:

  • Taifa Stars inakabiliwa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia, mwezi ujao katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wakati kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kikitangazwa jana na kuondoka leo kwenda Saudi Arabia kitakapocheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Sudan, idadi kubwa ya nyota wanaocheza timu mbalimbali za Ligi Kuu haijajumuishwa kikosini.

Uwepo wa mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la CRDB katika mwezi huu unaonekana kulazimisha benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya Juma Mgunda na Hemed Morocco kuita wachezaji watano tu ambao wapo kwenye vikosi vya timu zinazoshiriki Ligi Kuu huku majina mengi yaliyozoeleka yakikosekana.

Fursa kubwa inaonekana kutolewa kwa wachezaji wanaocheza timu zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar na wale wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.

Wachezaji watano walioitwa ambao wanacheza Ligi Kuu Bara ni Ally Salim wa Simba, Mukrim Abdallah (Ihefu), Abdulmalik Zacharia (Namungo), Baraka Mtuwi na Omary Abdallah (Mashujaa) pamoja na Khalid Idd wa Singida Fountain Gate.

Katika kikosi hicho, ameitwa pia kipa wa timu ya vijana ya Azam na kituo cha maendeleo ya ufundi Tanzania, Abrahman Vuai.

Kikosi kinaundwa na wachezaji 21 ambapo makipa ni watatu, mabeki saba, viungo watano na washambuliaji sita.

Makipa walioitwa ni Ally Salim, Ahmed Salula na Vuai wakati mabeki ni Mukrim, Alphonce Mabula, Miano Danilo, Gadiel Michael, Abdulmalik Zakaria, Baraka Mtuwi na Abddlrahman Bausi.

Viungo walioitwa ni Mohammed Sagaf, Morice Abraham, Khalid Idd, Isihaka Mwinyi na Jabir Mpanda wakati washambuliaji ni Omary Abdallah, Ben Starkie, Oscar Paul, Kelvin John, Tarryn Allarakhia na Ibrahim Ilika.