Martinelli aiokoa Arsenal na kipigo nyumbani
Muktasari:
- Arsenal inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 10.
Bao la dakika za nyongeza la Gabriel Martinelli limeinusuru Arsenal isipoteze nyumbani dhidi ya Man City katika mechi ya Ligi Kuu England iliyochezwa kwenye Uwanja wa Emirates, London England leo Septemba 21.
Licha ya Man City kucheza kwa kujilinda katika dakika nyingi za mchezo, ilijikuta ikifanya kosa la kumruhusu Martinelli kupokea pasi ya Eberechi Eze akiwa analitazama lango lao na mshambuliaji huyo kutoka Brazil alitumia vyema fursa hiyo kuubetua mpira uliompita kipa Gianluigi Donnarumma na kujaa wavuni.
Awali Manchester ilipata bao la mapema dakika ya tisa ya mchezo kupitia kwa Erling Haaland aliyemalizia vyema pasi ya Tijjani Reijnders.
Matokeo hayo yameifanya Arsenal irudi katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikifikisha pointi 10 huku Man City ikisogea hadi nafasi ya tisa ikifikisha pointi saba.
Kwa Arsenal, sare hiyo imeifanya iendeleze rekodi yake nzuri ya kutopoteza mechi dhidi ya Man City ambapo sasa imefikisha michezo sita mfululizo ambayo haijapoteza dhidi ya timu hiyo inayonolewa na Pep Guardiola.
Bao ambalo Erling Haaland amefunga leo, limemfanya afikishe idadi ya mabao matano aliyopachika katika mechi saba za Ligi Kuu ya England dhidi ya Arsenal.
Na Martinelli kwa upande wake, hili ni bao la pili ambalo amefunga dhidi ya Manchester City katika Ligi Kuu ya England, kwenye mechi tisa alizowahi kukutana nayo.
Matokeo ya sare yameonekana kutawala katika Ligi Kuu ya England leo kwani hata mechi nyingine mbili nazo zimemalizika kwa sare.
Bournemouth ambayo ilikuwa nyumbani, imelazimishwa sare tasa na Newcastle United huku Sunderland ikitoka sare ya bao 1-1 na Aston Villa.
Bao la Aston Villa lilifungwa na Matty Cash na lile la Sunderland limepachikwa na Wilson Isidor.