Malima asoma ujumbe wa Rais IOC miaka 130 ya Olimpiki

Muktasari:

  • Mbio hizo ziliongozwa na Malima, aliyesoma ujumbe wa kiongozi huyo mkuu wa IOC uliosema," maadhimisho ya Siku ya Olimpiki mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa nchi mwanachama zinajiandaa na michezo ijayo ya Paris 2024.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesoma ujumbe wa Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) Thomas Bach.

Bach ametuma ujumbe huo kwa nchi mwanachama wa IOC ikiwamo Tanzania ambayo leo Juni 23, 2024 imeadhimisha miaka 130 ya IOC kwa kushiriki mbio za kilomita 2.5 na za kilomita tano zilizoanzia na kumalizikia kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mbio hizo ziliongozwa na Malima, aliyesoma ujumbe wa kiongozi huyo mkuu wa IOC uliosema," maadhimisho ya Siku ya Olimpiki mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa nchi mwanachama zinajiandaa na michezo ijayo ya Paris 2024.

"Michezo ambayo kwa mara ya kwanza itazingatia idadi sawa ya washiriki wa jinsia zote, ikiendeleza kauli mbiu ya Olimpiki ambayo ni daraja la kuwaunganisha watu pamoja katika amani, utu na mshikamano," ulisomeka hivyo ujumbe huo.

Akihitimisha kusoma ujumbe huo, Malima ambaye leo amewaongoza mamia ya wadau wa michezo kushiriki kwenye maadhimisho hayo ya kitaifa, amesema ni ujumbe ambao unamgusa kila mmoja katika tukio hilo ni la kihistoria.

Amesema, Tanzania pia ni miongoni mwa nchi zitakayoshiriki michezo hiyo baada ya wanariadha wake, Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu kufikia viwango.

"Tunaamini wanamichezo wetu watafanya vizuri, lakini pia mkoa wa Morogoro tumepata bahati, kwani katika maadhimisho haya washiriki siyo tu wametoka Halmashauri ya mji wa Morogoro, la hasha, wapo wengine kutoka nje ya Mkoa wetu.

"Wameungana na wanamichezo, wanafunzi, walimu, viongozi na wananchi kutoka Wilaya zetu za Ulanga, Kilombero, Kilosa, Mvomero, Morogoro Vijijini na mwenyeji Morogoro mjini kushiriki katika tukio hili la kihistoria katika Olimpiki," amesema.

Amesema, maadhimisho hayo ni fursa nyingine kwenye mkoa huo ambao una historia ya kutoa vipaji vya michezo hususani soka akitaka wadau wa michezo mkoani humo kuitumia siku hiyo kimkakati katika kuendeleza zaidi michezo mkoani humo.

Malima pia amegusia mafunzo ya utawala na uongozi wa michezo yaliyoandaliwa na TOC kwa udhamini wa kitengo cha misaada cha IOC (Olympic Solidarity) yaliyowahusisha walimu na viongozi wa baadhi ya vyama vya michezo vya mikoa akieleza namna yatakavyoasaidia kuendeleza vipaji.

"Nawakumbusha wanamichezo wa Morogoro tuendelee kuutangaza mkoa wetu katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya kimichezo ambayo sasa ina fursa ya ajira," amesema.

Akitoa historia ya IOC, Katibu mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema iliundwa na watu saba wakiongozwa na mwanafalsafa Pierre de Coubertin, siku kama ya leo mwaka 1894 huko Paris, Ufaransa.

"Tangu wakati huo,  kila mwaka siku hiyo huadhimishwa na Kamati za Olimpiki za Kitaifa (NOC) zaidi ya 200 ambazo ni mwanachama wa IOC, Tanzania ikiwa mojawapo," amesema.

Amesema wanaadhimisha siku hiyo kila mwaka kwa kushiriki shughuli mbalimbali za michezo kwa kushirikiana na Serikali za Mikoa na vyama vya michezo katika mkoa husika.