RC Malima aagiza zimamoto kuchunguza ajali iliyoua 11 Kiwanda cha Sukari Mtibwa

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima wa kwansa kushoto alipofika Hospitali ya Mtibwa kutoa pole kwa wafiwa katika ibada fupi ya kuaga miili. Picha na Johson James

Muktasari:

  • Baadhi ya miili ya waliofariki kutokana na ajali hiyo imeanza kuchukuliwa na ndugu kwa ajili ya maziko.

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema Jeshi la Zimamoto litatumia siku tatu kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mlipuko uliotokea katika Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine wawili kujeruhiwa.

Malima pia ameshiriki Ibada fupi ya kuaga baadhi ya miili ya wafanyakazi hao iliyokuwa imehifadhiwa katika hospitali ya kiwanda ambayo imekabidhiwa kwa ndugu zao.

“Jeshi la Zimamoto litatumia siku tatu kufanya uchunguzi wa sababu za ajali hii iliyoua ndugu zetu 11,” amesema.

Wakati huohuo, mkuu huyo wa mkoa amesema kiwanda hicho kitafungwa kwa siku tatu ili pia zitumike kwa maombolezo.

“Pia kiwanda kimesema kitagharamia mazishi kwa kila familia, na baada ya msiba Serikali kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu itakaa pamoja na kiwanda ili kujua wanapataje fidia baada ya ndugu hao kufariki dunia wakiwa kazini,” amesema Malima.

kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TPAWU) Kanda ya Morogoro, Nichoraus Ngowi amesema taarifa za ajali hiyo wamezipokea kwa mshtuko mkubwa.

“Tunafikiri huenda sisi wafanyakazi hatuko salama kutokana na ajali zinavyotokea, lakini kwa kuwa imeshatokea, hatuna budi kuungana na familia katika maombolezo ya ndugu zetu hawa,” amesema Ngowi.

Ameziomba mamlaka za viwanda kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wawapo kazini ili kuepusha majanga kama hilo lililotokea.


Mtoto wa marehemu

Jodack David ni mtoto wa marehemu Majaliwa Mbena aliyefariki dunia kwenye ajali hiyo, amesema baba yake alifanya kazi kwenye kiwanda hicho kwa miaka 35, kwenye  kitengo cha kufua umeme .

“Taarifa za kifo cha baba tumezipata usiku baada ya kupigiwa simu na wafanyakazi wenzake, tukaja kiwandani usiku huohuo na kukuta ni kweli baba amefariki, maziko yake yatafanyika Kilosa kesho mchana.”

 “Mwili umeshaandaliwa kwa ajili ya kuanza safari jioni hii kwenda Kilosa, tumepata pigo kubwa kwenye familia, hatujui tuseme nini kwa sasa,” amesema.


Waliofariki

Majaliwa Egdy Mbena, Michael Mpoli, Thomas Nthenge, Caleb Mshani, Ally Waziri, Nalayanassamy, Diamwale Aziz, Ramadhani mbilu, Juma abdul, Eric mpokwa, Sergio Santos (Brazilian),