Manusura wasimulia mtambo wa joto ulivyoua 11 kiwanda cha Sukari Mtibwa

Sehemu ya mitambo ya kiwanda cha sukari Mtibwa. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Wakisimulia chanzo cha ajali hiyo, wafanyakazi walionusurika wamesema chanzo ni kupasuka bomba la joto na kuwaathiri wafanyakazi wenzao waliokuwa kwenye chumba cha uendeshaji mitambo.

Morogoro. Baadhi ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kilichopo Tuliani, Morogoro wameeleza jinsi bomba linalozalisha mvuke wa joto lilivyolipuka na kusababisha vifo vya wenzao 11 na wengine kujeruhiwa.

Alfajiri leo Mei 23, 2024 wakati wakijiandaa kuanza uzalishaji kiwandani hapo, ndipo bomba hilo linalopokea mvuke wenye joto kali limelipuka na kuwaathiri waliokuwa kwenye chumba cha uendeshaji mitambo.

Meneja wa umeme katika kiwanda hicho, Juma Balanda amesema imetokea hitilafu iliyosababisha bomba hilo kulipuka.

“Ajali imetokea baada ya bomba la kupokea mvuke wa joto ambalo linafikia nyuzijoto 450 kupasuka na lile joto kuwazidi wale watumishi na kufariki dunia.

“Awali tulikuwa na shughuli ya maboresho kwenye mitambo yetu kwenye mfumo wa kusafirisha joto, hivyo kabla ya kuanza uzalishaji rasmi, ndio ukatokea mpasuko ambao umeleta madhara haya.

“Waliofariki ni watu 11, katika hao mmoja ni raia wa Brazil ambaye alikuwa fundi mkuu, mwingine ni raia wa Kenya ambaye ni mtaalamu wa umeme, mwingime ni raia wa India ambaye ndiye alikuwa meneja na wengine wanane ni Watanzania,” amesema.

Amesema chumba kilikuwa na wataalamu na waendeshaji waliofikia 16, mmoja alitoka kwenda chumba kinachochochea joto, yeye alitoka nje kuzungumza na simu na mtumishi mwingine alimkuta nje.

Balanda amesema wakati wako nje, ukatokea mlipuko kwa sauti kubwa, moshi mkubwa ulitanda na vijana wawili wakatoka wakiwa na hali mbaya, kwa kuwa joto lilikuwa kubwa na kilichowasaidia ni kwamba mvuke haukuwapiga moja kwa moja lakini waliungua ngozi ya juu.

“Nilikuwa nimechanganyikiwa lakini baadaye nikawachukua, nikawawahisha hospitali. Wakati narudi kutoka hospitali, nikaona miili ya watu imelala, wote wakiwa wameshafariki dunia,” amesema meneja huyo.

Manusura mwingine wa ajali hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, ameliambia Mwananchi kuwa yeye aliingia kazini Mei 22, 2024 kuanzia asubuhi hadi saa 3 usiku muda wa kutoka.

“Jana, shifti yangu ilikuwa asubuhi hadi saa 3 usiku, nilipotoka kwenda nyumbani nikapigiwa simu baada ya kumaliza kuoga nirudi kazini, maana kulikuwa na majaribio ya mitambo ili tuanze uzalishaji, nikakubali.

“Nikarejea, nilipofika tukaanza majaribio lakini wakati hatujaruhusu ule mvuke uanze kusambaa kwenye mtambo wake, ndipo bomba likapasuka na mimi nilikuwa chumba cha pili sikupata madhara yoyote, kwa kuwa joto lile linafikia nyuzijoto 450 halikunifikia, basi wale tuliokuwa nao wakafariki baada ya mlipuko huo,” amesema.

Kwa upande wake, fundi mwingine ambaye ni fundi mkuu wa kitengo linapozalishwa joto la kuendesha mtambo huo, ambaye pia hakutaka kutaja jina lake, amesema ni kama bahati kwake kuwa hai.

“Ule mtambo ulikuwa unatengenezwa, tulianza majaribio tangu jana mchana, kila tukijaribu haukubali, sasa tukatengeneza mara ya mwisho kwa ule usiku ili tujaribu kwa mara ya mwisho, tukafunga kila kitu, tukaanza kuzalisha joto ili lifikie 450, kisha tuliruhusu kwenda panapohusika ili tujaribu tuone kama joto na presha vinapanda kwa pamoja.

“Kabla kiwango cha joto tulichotaka hakijafika, ghafla nikasikia mlipuko mkubwa, kumbe kuna bomba lilizidiwa na kupasuka, basi wenzetu wakafariki katika mazingira hayo na mimi nilikuwa upande mwingine,” amesema.

Mganga mfawidhi katika Hospitali ya Turiani, David Ruchwaisa amesema wamepokea majeruhi wawili kutoka kwenye ajali hiyo.

“Tumepokea wagonjwa wawili kutoka kwenye ajali ya kiwanda cha Mtibwa na tumewapa huduma ya kwanza lakini kwa hali zao tunaandaa rufaa ili wasafirishwe kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma ili wakatibiwe huko.

“Wamepata majeraha sehemu tofautitofaut ikiwemo uso, kifua, tumbo, mgongo, mikono na miguu, hali zao sio nzuri sana, lakini naamini kadri wanavyopata matibabu, afya zao zitaimarika,” amesema.

Mwananchi Digital imefika ilipo hospitali ya Kiwanda cha Mtibwa na kushuhudia umati wa watu ambao miongoni mwao ni ndugu wa marehemu waliofika kutambua miili ya ndugu zao, ambapo maofisa wa Jeshi la Polisi waliwasihi wananchi hao kuwa wavumilivu ili uchunguzi ukikamilika wapewe miili kwa ajili ya taratibu wa mazishi.

Wakati huohuo, shughuli kwenye kiwanda hicho zimesimama kwa muda baada ya kutokea kwa hitilafu hiyo na uzalishaji utaanza baada ya uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo kukamilika na taratibu zingine kuhusu ajali hiyo.