Madeni matatu Taifa Stars ikishuka dimbani leo
Beki wa Kulia wa Taifa Stars, Haji Mnoga wakati akijaribu kuwatoka wachezaji wa Liechtenstein katika mechi ya kirafiki ya FIFA Series 2026 iliyofanyika katika Uwanja wa Pele, Kigali, Rwanda, Machi 26, 2026. Picha na Tanfootball
Kigali, Rwanda. Taifa Stars leo inahitimisha mashindano ya FIFA Series 2026 kwa kukabiliana na Macau katika Uwanja wa Pele, Kigali kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki.
Mambo matatu yanailazimisha Taifa Stars kupata ushindi katika mchezo huo wa kuwania nafasi ya tatu ya kundi lao la Rwanda B ambao utafuatiwa na fainali baina ya Liechtenstein na Aruba.
Kwanza ni kufuta aibu ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya vibonde Liechtenstein katika mechi ya kwanza Alhamisi iliyopita, licha ya Taifa Stars kupewa nafasi kubwa ya kupata ushindi katika mechi hiyo.
Deni la pili kwa Taifa Stars leo ni kumaliza nuksi ya muendelezo wa matokeo yasiyovutia ambayo imeonekana kuyapata mfululizo licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi.
Taifa Stars haijapata ushindi katika mechi 11 mfululizo zilizopita hivi karibuni za mashindano tofauti ambapo imetoka sare nne na kutoka sare katika michezo saba.
Jambo la tatu ambalo linaiweka Taifa Stars katika ulazima wa kupata ushindi leo ni kuzuia isiporomoke zaidi katika chati ya viwango vya ubora wa soka ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vitakavyotolewa Aprili Mosi mwaka huu.
Tayari kichapo cha bao 1-0 ambacho Taifa Stars ilikipata Alhamisi iliyopita kutoka kwa Liechtenstein kimeishusha kwa nafasi tatu kutoka ya 110 hadi ya 113 kwa mujibu wa mabadiliko ya chati hiyo kwa mwezi Machi hivyo kupoteza leo kunaweza kuifanya iporomoke zaidi.
Macau yenyewe inaonekana sio mpinzani mgumu kwa Taifa Stars kwani ilianza mashindano hayo kwa kuchapwa mabao 4-1 na Aruba na haijapata ushindi katika mechi 12 zilizopita ambazo ilitoka sare moja na kupoteza 11 huku ikifunga mabao matatu tu na kufungwa mabao 27.
Utulivu na umakini katika kutumia nafasi zinaweza kuwa silaha mbili za kuibeba Taifa Stars leo na kutorudia kilichotokea katika mchezo uliopita ambao safu yake ya ushambuliaji ilipoteza nafasi nyingi ambazo ingezitumia chache tu ingeweza kupata ushindi dhidi ya Liechtenstein.
Wakati Taifa Stars ikiingia katika mechi hiyo huku ikiwa katika nafasi ya 113 kwenye chati ya viwango vya ubora wa soka duniani, Macau yenyewe ipo katika nafasi ya 194.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu hizo zikitoka sare katika dakika 90 za mchezo, mikwaju ya penalti itafuata katika kuamua mshindi.
Baada ya mchezo huo, kuanzia saa 1:00 usiku, Liechtenstein itakabiliana na Aruba katika mchezo wa fainali ambao nao utachezwa katika Uwanja huohuo wa Pele.