Ligi Kuu Bara kuboreshwa, neema zatajwa

Dar es Salaam. Tayari klabu ya Yanga jana imekabidhiwa kombe la Ligi Kuu likiwa na la 30 kwa klabu hiyo huku mdhamini mkuu akiahidi maboresho zaidi katika miaka minne iliyobakia.
Mdhamini wa Ligi Kuu Bara ambao ni benki ya NBC kupitia Mkuu wa Idara ya Masoko, David Raymond pamoja na kuipongeza timu ya Yanga SC kwa kuibuka kinara wa ligi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa miongoni mwa timu shiriki, alisema wataendelea kubuni mikakati mikubwa zaidi ya kuiboresha ligi hiyo ili kufikia malengo ya udhamini wake ambayo ni pamoja na kukuza vipaji na viwango vya soka nchini, kuchochea ajira kupitia michezo, kuongeza ushindani baina vilabu shiriki na kuongeza hamasa ya mchezo huo nchini.
“Kila mtu ni shuhuda wa mapinduzi makubwa ambayo tayari NBC tumeyafanya katika misimu hii mitatu ya udhamini wetu kwenye ligi Kuu na mwaka mmoja wa udhamini wetu kwenye ligi ya Championship na ligi ya Vijana.’’ alisema na kuongeza;
“Mbali na kuchochea ushindani kwenye ligi hizi kupitia udhamini ulioviweza vilabu shiriki kufanya usajili mzuri pia tumekuwa tukitoa huduma muhimu kwa timu hizi ikiwemo bima ya afya, mikopo ya usafiri kwa timu na zaidi tunahakikisha tunaandaa mazingira mazuri zaidi ya kuwakabidhi vikombe vyao vya ubingwa kwa kushikiriana na vilabu husika kuandaa matukio makubwa yenye kuongeza mvuto kwa mashabiki wao,’’ alisema Raymond akitolea mfano tukio la kuandaa helikopta maalum kwa ajili ya kuwasilisha kombe la ubingwa kwa klabu ya Yanga SC kwenye Uwanja huo.
Kwa mujibu Raymond udhamini wa benki hiyo kwenye ligi hizo umeambatana na matokeo chanya hata nje mchezo husika ambapo kupitia mnyororo wa sekta ya mchezo benki hiyo imeweza kuzalisha ajira za takribani 7,000 kupitia udhamini huo.
“Ni matokeo chanya kama haya ya ongezeko la ajira na hamasa ya mchezo huu ndivyo vinavyotupa msukumo zaidi wa kuendelea kubuni mikakati mikubwa zaidi ili kupamba zaidi udhamini wetu. Tunaamini katika miaka hii minne iliyosalia katika udhamini wetu tutakuja na mambo mazuri na makubwa zaidi ikiwemo kubuni huduma bora za kibenki zinazolenga kuhudumia na kutatua changamoto za vilabu vinavyoshiriki ligi hizi,’’ alisema Raymond