Kisa hasara, mastaa Chelsea kupigwa bei

London, England. Chelsea inajiandaa kuwapiga bei baadhi ya nyota wake katika dirisha la usajili lijalo ili kuepuka kukutana na rungu la sheria ya matumizi ya fedha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa).
Hilo limefichuliwa juzi na kocha wa timu hiyo, Graham Potter huku wachezaji walioripotiwa kuuzwa ni Mason Mount, Mateo Kovacic, Christian Pulisic na Hakim Ziyech. Inaripotiwa sababu ya kuwapiga bei mastaa hao ni kufidia hasara ya takribani Pauni 120 milioni ambayo imepata kutokana na matumizi mbalimbali lakini pia iwapo itakosa tiketi ya kushiriki mashindano ya Ulaya msimu ujao.
Potter ambaye timu yake imekuwa na mwenendo usioridhisha katika Ligi Kuu ya England msimu huu, alisema licha ya mahitaji yake kwa wachezaji hao atalazimika kuachana nao ili kunusuru klabu na suala hilo liko nje ya uwezo wake.
“Hiyo ndio changamoto tuliyo nayo. Tuna kikosi kikubwa kilichokamilika chenye wachezaji wengi wazuri. Vitu hivi vinachanganya kwa sababu havitokani na maoni yangu. Ni kuhusu mchezaji, klabu na vitu vingi. Sipo katika kuliamria hilo,” alisema.
“Kikubwa nachoweza kufanya ni kutoa maoni kwa Mason kama mwanasoka na mtu sina kingine zaidi ya kusema mambo chanya kuhusu yeye.” Kocha huyo alisema kuhusu Kovacic yeye anatamani kuendelea kuwa naye klabuni lakini mwisho wa siku mamlaka ya kuamua hilo hayako katika mikono yake.
“Nina heshima kubwa pia kwa Mateo. Anatimiza jukumu kwa ajili ya timu na amekuwa nahodha pia. Lakini inabaki kwa Mateo na klabu. Sio ulimwengu mzuri na unashughulika na kile unachopaswa kushughulika nacho katika msimu wa joto na kufanya maamuzi,” alisema.
Potter alisisitiza jukumu lake ni kuhakikisha anafanya kile ambacho ni sahihi kwa klabu pasipo kuhofia mtu yeyote huku akikiri kuwa anatamani kufanya kazi na nyota wake aliye kwa mkopo Inter Milan, Romelu Lukaku.
“Anatakiwa kumaliza msimu vizuri na kisha tutakuwa na uamuzi wa kufanya. Ni mtu mmoja ninayempenda na kuvutiwa naye vilivyo lakini ni kitu cha kuongea wakati wa majira ya kiangazi,” alisema Potter.
Uamuzi wa Chelsea kuwauza Mount na Kovacic huenda ukainufaisha Bayern Munich ambayo inatajwa kuwatamani viungo hao ili kuwaunganisha na kocha wao wa zamani, Thomas Tuchel ambaye amejiunga nao wiki iliyopita.
Timu nyingine ambayo imekuwa ikiwania huduma ya Mount na Kovacic ni Liverpool ambayo ina mpango wa kuimarisha safu yake ya kiungo katika usajili wa majira ya kiangazi.