Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KenGold, Yanga uzito tofauti

Muktasari:

  • Kwa upande wa KenGold, mechi nne za ligi ilizocheza msimu huu imepoteza zote ikifunga mabao mawili na kuruhusu nane. Inashika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi kuu ikiwa haina pointi.

Mbeya. KenGold ambayo hivi karibuni iliachana na kocha wake mkuu, Fikiri Elias na msaidizi wake Luhaga Makunja, leo inaingia kinyonge kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kuanzia saa 10:00 jioni ikiwa mwenyeji wa Yanga katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu.

Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na mwanzo mzuri msimu huu katika mashindano yote kwani imeshuka dimbani mara saba na kushinda mechi zote.

Katika mechi hizo saba ilizocheza Yanga ambapo mbili ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara (1) na Ligi ya Mabingwa Afrika (4), imefunga jumla ya mabao 24 na kuruhusu moja pekee.

Kwa upande wa KenGold, mechi nne za ligi ilizocheza msimu huu imepoteza zote ikifunga mabao mawili na kuruhusu nane. Inashika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi kuu ikiwa haina pointi.

KenGold ambayo hivi sasa inanolewa na Kocha Jumanne Charles akisaidiana na Aswile Asukile wana kazi kubwa ya kufanya kuizuia Yanga lakini pia kuisaka pointi ya kwanza ligi kuu.

Timu hiyo yenye maskani yake Chunya mkoani Mbeya, inamtegemea zaidi mshambuliaji wake Joshua Ibrahim ambaye ndiye aliyefunga mabao mawili waliyonayo kikosini hapo.

Mabeki wao akiwamo Ambukise Mwaipopo, Asanga Stalon, Makenzi Kapinga, Salum Iddrisa, Bila Amin, Martin Kazila na Charles Masai ambao wameonekana kucheza mechi zilizopita, wana kazi kubwa ya kuizuia safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Yanga imekuwa na kawaida ya kuwatumia viungo zaidi katika kutengeneza na kufunga mabao, hivyo wapinzani wanapaswa kuwa makini zaidi kuwazuia.

Unapoutaja Uwanja wa Sokoine, kwa Yanga wala haiwashtui kwani wana rekodi nao nzuri kwani mechi tano za mwisho ilizokwenda kucheza hapo na timu tatu tofauti ndani ya ligi, haijapoteza hata moja.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa tamaa yake ni kuona timu yake inapata ushindi pasipo kuzingatia idadi ya mabao.

"Mimi kiu yangu ni Yanga kupata pointi tatu hata kwa bao moja ni sawa, ila kama tutapata nafasi ya kufunga zaidi tutafanya hivyo na itakuwa nzuri zaidi, nimewaandaa vyema wachezaji wangu," alisema Gamondi.

Kocha wa KenGold, Jumanne Challe alisema kuwa Yanga isiingie na matokeo mfukoni kwani wanaweza kuwashangaza.

"Yanga nimeiona ubora na udhaifu wake, wanatumia sana mipira ya kushtukiza, injini yao ni kiungo, yule Mudathir na mabao yake ya mwishoni tutambana, bahati nzuri namjua vyema, kesho hawatapita," alisema Challe.