Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kabudi apewa Mwana FA, Makonda Wizara ya Michezo, wadau wapongeza

Muktasari:

  • Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amelitangaza leo Jumatatu, Novemba 17, 2025, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.Mawaziri wote wataapishwa kesho Jumanne.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemteua tena Profesa Palamaganda Kabudi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Uteuzi huo umetangazwa leo Jumatatu, Novemba 17, 2025 Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.

Kama alivyofanya kwa Kabudi, Rais Samia amemteua tena Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Wizara hiyo imeongezewa Naibu Waziri mmoja ambaye atakuwa ni Paul Makonda.

"Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri ni Profesa Palamaganda John Kabudi, Naibu Waziri ni Hamis Mwinjuma au maarufu Mwana FA na Naibu wa Pili ni Mheshimiwa Paul Christian Makonda," amesema Rais Samia.

Kibarua kikubwa cha Wizara hiyo ni maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ambazo zitafanyika hapa nchini mwaka 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Hapana shaka uzoefu wa Kabudi na Mwana FA katika maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 utakuwa msaada mkubwa kwa Makonda ambaye ni mpya katika wizara hiyo. Wadau tofauti wa Michezo wameonyesha kukoshwa na uteuzi huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Pamba Jiji FC, Alhaji Majogoro amesema kuwa uteuzi uliofanywa na Rais Samia katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, utakuwa na faida kubwa kwa sekta ya michezo.

"Uteuzi uko vizuri maana hawajabadili ile safu iliyokuepo. Kuongezeka kwa Makonda kunafanya iwe 'active' zaidi maana ni mfuatiliaji sana. Viwanja vitatembelewa mchana na usiku," amesema Majogoro.

Kocha wa Riadha, Denis Malle amesema ana imani kubwa na Waziri na Manaibu Waziri walioteuliwa katika Wizara hiyo.

"Binafsi wote nawakubali sana pia nina imani kubwa sasa  michezo ipo mikono salama zaidi. Mheshimiwa Waziri Kabudi hanaga mchezo katika masuala ya maendeleo,akisaidiwa majukumu na vijana machachari Mwinjuma na Makonda.

"Tuna kila sababu ya kutegemea ufanisi katika michezo. Ombi langu kwa Mh. Kabudi, waweke nguvu katika michezo ambayo ni gharama rahisi kuwekeza kama vile Riadha.

"Kwani Riadha hata mchezaji mmoja anaweza kuwakilisha nchi Kimataifa," amesema Kocha Malle.