JKT Tanzania yaivuta shati Yanga, Singida yapasuka kwa KMC

Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya pointi 46 katika michezo 18.
Dar es Salaam. Yanga imeweka rehani uongozi wake wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya leo kulazimishwa sare tasa na JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Licha ya timu hizo kushambuliana kwa nyakati tofauti, safu za ulinzi kwa kila timu zilikuwa imara kuokoa hatari ambazo zilielekezwa na kufanya hadi filimbi ya mwisho ya refa Ahmed Arajiga ilipopulizwa timu hizo kutoka sare.
Kazi ya ziada katika kikosi cha JKT Tanzania imefanywa na beki Wilson Nangu ambaye aliokoa hatari nyingi za washambuliaji wa Yanga jambo lililomfaidisha baada ya mechi kumalizika kwa kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 46 na kuendelea kuongoza msimamo wa ligi ingawa inaweza kupitwa na Simba ikiwa itapata ushindi dhidi ya Tanzania Prisons, kesho Februari 11 katika Uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amewapongeza wachezaji wake.
“Niipongeze timu na wachezaji. Hatukuwa na muda mwingi wa mazoezi tangu tumetoka Arusha. Tumecheza mechi tatu ndani ya wiki moja sio rahisi. Kikubwa niseme Yanga ni timu bora Tanzania na Afrika.
“Kupata pointi dhidi ya timu kubwa sio rahisi. Kama tutakuwa na kasi hii katika mechi nyingine, itakuwa vizuri. Pointi moja kwangu ni kitu kizuri,” amesema Ahmad.
Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud amesema kuwa ameridhika na matokeo ingawa hakufurahishwa na maamuzi ya refa.
“Tulijua sisi ni timu kubwa. Kila timu inapocheza na sisi lazima ijipange vilivyo. Sitaki kuzungumza kuhusu refa lakini kiukweli sina furaha kuhusu refa. Muda mwingi alisimamisha mchezo.
“Najua nini naongea. Bora kuwa katika nafasi ya pili na kwenda katika nafasi ya kwanza kuliko kuwepo katika nafasi ya kwanza halafu unarudi katika nafasi ya pili. Sio rahisi kushinda mechi zote,” amesema Miloud.
Katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, KMC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Singida Black Stars.
Mabao yote mawili katika mchezo wa leo yamefungwa na Oscar Paul huku Singida Black Stars ikipoteza mkwaju wa penalti uliokoswa na
Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma amesema kuwa hawakuwa na bahati katika mchezo huo.
“Hatukuwa na haraka ya kuingia katika boksi lao. Muundo ambao tulikuwa nao ni tulitaka kuwa na balansi nzuri. Leo tumefungwa magoli mepesi. Imekuwa ni bahati mbaya kwetu tukapata penalti tukakosa.
“Tumepata nafasi mbili ambazo KMC wameokoa kwenye mstari kwa hiyo tulikosa bahati. Ukweli ni kwamba sasa hivi tunapata nafasi nyingi hivyo tunahitajika kuzitumia kama tukiwa na uwezo wa kuzibadilisha kuwa magoli itanisaidia,” amesema Ouma.
Kocha wa KMC, Kally Ongala amesema amefurahishwa na matokeo ya mchezo huo.
“Napenda kuwapongeza wachezaji wangu. Tumecheza mechi mbili kwa ukaribu na zote tumeweza kutawala. Nawapongeza kwa kipindi cha pili wameweza kujilinda vyema na Singida hawakupata bao japo walikuwa wanatupa presha.
“Tunahitaji wachezaji wanaoweza kuokoa. Nimeridhishwa na kiwango cha timu. Tulihitajika kuwa watulivu na kucheza kwa staili yetu,” amesema Ongala.