Jeraha lamweka Odegaard nje wiki nane Arsenal
Muktasari:
- daktari Lars Engebretsen amesema huenda nyota huyo akawa nje kwa muda wa wiki sita hadi nane.
London, England. Habari mbaya zimewapata mashabiki wa Arsenal baada ya daktari wa zamani wa timu ya taifa ya Norway kufichua kuwa nahodha wao, Martin Odegaard, anaweza kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kufuatia jeraha la goti alilopata mwishoni mwa wiki.
Odegaard alilazimika kutoka nje ya uwanja katika dakika ya 30 kwenye mchezo dhidi ya West Ham United baada ya kugongana goti kwa goti na Crysencio Summerville.
Kiungo huyo aliondoka Emirates akiwa amefungwa kifaa maalum kwenye goti la kushoto, na vipimo vilibaini kuwa amepata majeraha kwenye mishipa ya ndani ya goti.
Ingawa Arsenal hawajatoa muda rasmi wa mapumziko, daktari Lars Engebretsen, ambaye aliwahi kuhudumu na timu ya taifa ya Norway, amesema huenda nyota huyo akawa nje kwa muda wa wiki sita hadi nane.
“Nimeangalia video ya tukio. Inaonekana kama jeraha la mishipa ya pembeni ya goti. Ikiwa ndivyo, anaweza kuwa nje kwa wiki 6 hadi 8, lakini inategemea ukubwa wa tatizo,” amesema Engebretsen akizungumza na gazeti la Dagbladet.
“Pia kuna uwezekano jeraha hilo likawa kubwa zaidi, likahusisha mishipa mikuu ya goti. Hapo itachukua muda mrefu zaidi kurejea.”
Kwa sasa, Odegaard (26) ameingia kwenye historia isiyotakiwa katika Ligi Kuu England, baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kutolewa nje kabla ya mapumziko katika mechi tatu mfululizo.
Awali alishindwa kumaliza michezo dhidi ya Nottingham Forest na Leeds United kutokana na maumivu ya bega yaliyokuwa yanamsumbua.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema nahodha wake ana hofu kubwa kwamba jeraha hili jipya linaweza kuwa baya zaidi.
“Nimezungumza naye, na hajisikii vizuri kuhusu hali yake. Kwa hiyo tunasubiri ripoti kamili kutoka kwa madaktari.
“Tulikuwa hatujabahatika sana msimu huu amekosa michezo mingi tangu mwanzo kutokana na bega, sasa tena goti. Tutasubiri kuona ukubwa wa tatizo, lakini ni wazi yeye ni mchezaji muhimu sana. Anatupa ubunifu mkubwa hasa eneo la ushambuliaji,” amesema Arteta baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya West Ham.
Baada ya mapumziko ya michezo ya kimataifa, Arsenal itasafiri kumenyana na Fulham, kisha kuwakaribisha Atletico Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, kabla ya kuvaana na Crystal Palace.
Akizungumzia ratiba hiyo, Arteta alisema:
“Tunajua mechi hizo zitakuwa ngumu, hasa baada ya kipindi hiki cha mapumziko. Tumepita katika changamoto kubwa tulicheza dhidi ya timu ngumu, zingine zikiwa ugenini, na tumekuwa na majeraha mengi.
“Lakini wachezaji wameonyesha ubora mkubwa na matokeo mazuri. Huu ni msingi mzuri kuendelea mbele.”