Jamie Vardy aondoka Leicester City na mabao 200

Muktasari:
- Vardy amecheza mechi yake ya mwisho jana kwenye Uwanja wa King Power dhidi ya Ipswich Town akiwa amedumu klabuni hapo kwa miaka 13 tangu alipojiunga mwaka 2012.
London, England. Mshambuliaji wa Leicester City, Jamie Vardy amepewa mkono wa kwaheri na timu yake baada ya mchezo wa jana kumalizika Leicester City ilipokuwa nyumbani dhidi ya Ipswich Town kwenye Uwanja wa King Power.

Katika mchezo huo Leicester City iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku Vardy akifunga bao kwenye mchezo huo. Mshambuliaji huyo raia wa England alifunga bao la kuongoza katika dakika ya 28 huku bao lingine likifungwa na Kasey McAteer katika dakika ya 69 Leicester ikiondoka na ushindi.

Vardy mwenye umri wa miaka 28, ameichezea Leicester City jumla ya michezo 500 katika mashindano yote huku akifunga jumla ya mabao 200 tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2012 akitokea Fleetwood Town.
Anaondoka Leicester City akiwa mfungaji wa tatu bora wa muda wote na mchezaji wa tatu aliyecheza mechi nyingi zaidi katika historia ya klabu na amekuwa mhimili wa mafanikio ya timu hiyo.

Katika msimu wa 2014/15, aliisaidia Leicester City kushinda taji la Ligi Kuu ya England jambo linalotajwa kuwa moja ya mafanikio makubwa kabisa katika historia ya timu pamoja na mchezaji mwenyewe.
Katika msimu huo, Vardy alifunga mabao 11 kwenye Ligi Kuu na alitangazwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya England na mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo.

Aliendelea kufunga mabao katika michuano ya UEFA Champions League na UEFA Europa League katika misimu iliyofuata na pia kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu msimu wa 2019/20, baada ya kufunga mabao 23.
Mbali na kutwaa mataji mawili ya Championship akiwa na Leicester, nahodha huyo pia alisaidia timu yake kushinda Kombe la FA kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu mwaka 2021.

Kwa kufanya hivyo, alikuwa mchezaji wa kipekee katika historia ya timu hiyo kucheza michezo mingi jambo linalothibitisha bidii, kujituma na kipaji kilichomfikisha kileleni mwa soka.
Mwenyekiti wa Leicester City, Aiyawatt Srivaddhanaprabha, amesema:
“Jamie ni wa kipekee. Yeye ni mchezaji maalumu na hata zaidi, ni mtu wa kipekee sana. Anashikilia nafasi ya kipekee katika mioyo ya kila mmoja aliye na uhusiano na Leicester City, na bila shaka ana heshima na upendo wa dhati kutoka kwangu. Ninashukuru mno kwa kila kitu alichokitoa kwa klabu hii ya soka.

“Ingawa muda wa Jamie kama mchezaji wetu unafikia tamati, yeye na familia yake daima watakaribishwa kwa mikono miwili katika Uwanja wa King Power kwa kila walichofanikisha. Kwa niaba ya kila mmoja ndani ya Leicester City, namtakia Jamie na familia yake heri njema katika maisha yajayo, na najua mashabiki wetu wataungana nasi kumpa heshima anayostahili mwishoni mwa msimu huu,” amesema bosi huyo wa Leicester.

Mpaka sasa timu zilizoonyesha nia ya kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyu ni Everton na Leeds United za England. Timu nyingine ni Celtic na Rangers za Scotland huku kukiwa na tetesi kutoka katika timu za Ligi Kuu Marekani (MLS) kuhitaji huduma ya Vardy.