Ishu ya Kibu Simba iko hivi

Muktasari:
- Kikosi cha Simba imeingia wiki ya tatu ya kambi Misri bila mshambuliaji Kibu Denis, ambaye alipewa ruhusa kwenda Marekani.
Dar es Salaam. Wakati Simba ikiingia wiki ya tatu ya kambi yake ya maandalizi ya msimu ujao huko Ismailia, Misri bado nyota wake Kibu Denis hajaungana na kikosi cha timu hiyo huku uongozi ukisema haufahamu kwa nini bado mshambuliaji huyo hayupo na wenzake huko.
Awali Simba ilisema kuwa mchezaji huyo alipewa ruhusa ya kwenda mapumziko Marekani na ataungana na timu ikiwa Misri lakini jana Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa hadi sasa hawafahamu kwa nini mchezaji wao huyo hajaungana na wenzake Misri.
“Kibu anatakiwa awepo kambini lakini hayupo kambini. Wachezaji walitakiwa waripoti kambini tarehe 8 Julai lakini yeye hayupo na hatuna taarifa yoyote ya sababu za kutokuwepo kambini,” alisema Ally.
Msimamizi wa mchezaji huyo, Carlos Sylivester alisema kuwa atalitolea ufafanuzi suala hilo.
“Hilo suala nitalizungumzia naomba mnipe muda,” alijibu Sylivester.
Wiki iliyopita, Kibu alifanyiwa mahojiano akiwa Marekani ambapo alitupa mpira kwa viongozi wa Simba kuwa ndio wanaweza kulizungumzia suala hilo.
“Sina la kusema, we watafute viongozi,” alijibu Kibu.
Hivi karibuni, Kibu alisaini mkataba mpya wa kuitumikia Simba kwa muda wa miaka mitatu ambao inaripotiwa dau la usajili linafikia zaidi ya Shilingi 300 milioni.
Kibu alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Simba msimu uliomalizika ingawa alimaliza akiwa amefunga bao moja.
Katika Ligi Kuu msimu uliopita, Kibu alicheza mechi 21 kati ya 30 ambapo kati ya mechi hizo, mechi 17 alianza katika kikosi cha kwanza na nne aliingia akitokea benchi.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alicheza mechi zote 10 msimu uliopita kuanzia zile za hatua ya awali hadi robo fainali ambapo mechi tisa alianza katika kikosi cha kwanza na mchezo mmoja aliingia akitokea benchi.
Katika hatua nyingine uongozi wa Simba umemrejesha kikosini Patrick Rweyemamu kuendelea na majukumu yake ya kuwa meneja wa timu hiyo.
Rweyemamu anarudi kwenye nafasi hiyo baada ya msimu uliopita kuondolewa na kuwa Mkuu wa Programu za Soka la Vijana wa klabu hiyo.
Kurejea kwake anachukua nafasi ya Mikael Igendia raia wa Kenya ambaye alikuwa meneja wa timu hiyo na mkuu wa Sayansi ya michezo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwananchi kuwa ni kweli wameamua kumrejesha Rweyemamu ndani ya timu hiyo na jana jioni alisafiri kwenda Misri kwa ajili ya kuungana na timu.
“Rweyemamu leo (jana) amesafiri kuelekea Misri tayari kwaajili ya kuendelea na majukumu yake ndani ya timu yetu ambayo inaendelea kujiweka fiti tayari kwa msimu mpya,” alisema mtoa taarifa huyo.
Rweyemamu mbali na kushika nafasi tofauti za uongozi ndani ya Klabu ya Simba, aliwahi pia kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hasa zile zinazohusu soka la vijana.
Mwananchi lilipomtafuta Rweyemamu kwa ajili ya kuthibitisha taarifa hizo alisema suala hilo kama lina ukweli wowote taarifa itatolewa na Klabu ya Simba muda ukifika.
Kikosi cha Simba kilichoweka kambi Misri kuanzia Julai 8 mwaka huu, kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam siku chache kabla ya Agosti 3 kufanya Tamasha la Simba Day ambalo huu utakuwa ni msimu wa 16 tangu kuanzishwa kwake 2009.
Baada ya Simba Day, Simba itakaa takribani siku tano kabla ya kuvaana na Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Agosti 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 usiku.