Guede, Musonda wapewa mikoba Al Ahly

Muktasari:
- Muda mchache ujao mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly utaanza, huku timu zote zikiwa zimeshafuzu hatua ya robo fainali na zinatafuta nafasi ya kuwa kinara wa kundi.
Kikosi cha Yanga kinachoivaana Al Ahly kimewekwa hadharani, huku mshambuliaji Joseph Guede akianza na Maxi Nzengeli akianzia nje.
Muda mchache ujao mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly utaanza, huku timu zote zikiwa zimeshafuzu hatua ya robo fainali na zinatafuta nafasi ya kuwa kinara wa kundi.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika Guede anaanza, baada ya ule uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa wiki moja iliyopita kuanzia benchi, lakini alipoingia aliifungia timu yake bao la mwisho ambalo liliifanya ishinde 4-0 dhidi ya CR Belouazdad na kufuzu robo fainali baada ya kuisotea nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ameanzisha kikosi ambacho kinaonyesha kinakwenda uwanjani kushambulia baada ya kuanzia na washambuliaji wawili, Guede na Kennedy Musonda.
Kwenye eneo la kiungo, Gamondi ameanza na Khalid Aucho, Pacome Zouazou na Aziz KI huku langoni akianza Djigui Diarra, akisaidiwa na mabeki Yao Kouassi, Joyce Lomarisa, Dickson Job na Ibrahim Bacca ambao walianza pia kwenye mchezo uliopita.
Kama Yanga itafanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu, itakuwa ni mara yao ya kwanza kuifunga Ahly nyumbani.