Fuatilia hatua kwa hatua dili za moto kabla dirisha kufungwa Ulaya

Zimebaki saa chache kwa dirisha la usajili barani Ulaya kufungwa rasmi, lakini mawakala na wakurugenzi wa ufundi wako bize kuhakikisha wanawanasa mastaa wanaowahitaji ili kuimarisha vikosi vyao.
Katika Ligi Kuu England, vigogo Manchester United, Chelsea, Arsenal na Tottenham wapo kwenye harakati za kusaka vifaa vipya. Hizi hapa baadhi ya sajili zinazokaribia kukamilika na ambazo bado ngoma ngumu.
• Mathys Tel – Manchester United bado wanapambana kunasa saini ya mshambuliaji huyu kutoka Bayern Munich. Kinda huyu ya kifaransa kwenye miaka 19, yuko kwenye rada za kocha Ruben Amorin. Hata hivyo, Bayern Munich wanataka dau waliloweka lifikiwe kwanza.
• Ben Chilwell: Kwa sasa hana namba kwenye kikosi cha Chelsea na muda wowote anatarajiwa kutua Crystal Palace kwa mkopo. Taarifa zinasema mazungumzo binafsi yamekamilika na anatarajia kufanyiwa vipimo muda wowote kuanzia sasa.
• Marc Guehi: Dili lake la kutua Chelsea huenda likaota mbawa na kubaki kwenye klabu yake ya Crystal Palace. Palace wamegomea ofa nyingine ya Guehi kutoka Tottenham.
• Nico Gonzalez: Manchester City wako kwenye mazungumzo ya kunasa saini ya kiungo fundi wa Porto, Nico. Porto wameitaka Man City kufika dau la pauni 50 milioni.
• Axel Disasi : Tottenham imeanza kukata tamaa kuhusu mpango wake wa kuinasa saini ya staa wa Chelsea, Disasi. Kwa sasa Aston Villa wamebaki wenyewe kwenye mbio hizo.
• Christopher Nkunku : Manchester United wanahitaji huduma ya Nkunku, lakini dau ambalo Chelsea wameweka linaonekana kuwa kikwazo. Awali, kulikuwa na mpango wa kubadilishana na Alejandro Gernacho, ambaye yuko sokoni.
• Joao Felix : Jorge Mendes ametua jijini London kuangalia uwezekano wa kufanikisha dili la mteja wake, Joao kwenda kukipiga AC Milan kwa mkopo kutoka Chelsea. Mendes na mabosi wa Chelsea kwa sasa wako mezani.
• Lloyd Kelly : Juventus inapambana kukamilisha dili la kumnasa beki wa Newcastle, Kelly huenda akajiunga na Juventus kwa mkopo wenye kipengele cha kuuzwa jumla kwa dau la pauni 20 milioni.
#Update
Joao Felix anajiandaa kufanya vipimo kwa ajili ya kujiunga na AC Milan akitokea Chelsea kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita usio na kipengele cha kununuliwa moja kwa moja.
AC Milan itailipa Chelsea, Pauni 5 milioni huku ikikubali kulipa mshahara wote wa Felix.